Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji (kati) akizungumza na waandishi wa habari jan akuhusiana na ziara yao nchini Rwanda, kushoto ni makamu mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga na kulia ni Katibu wa Yanga, Mwesiga Selestine.
WAKATI mabingwa wa Kombe la
Kagame, Yanga, wakiondoka nchini jana kwenda Rwanda kwa mwaliko wa Rais wa nchi
hiyo, Meja Jenerali Paul Kagame, Rais Jakaya Kikwete ‘JK’ naye amewaalika Ikulu
kuwapongeza.
Rais Kagame, ametoa mwaliko
huo kuwapongeza baada ya kutwaa kombe hilo Julai
28, jijini Dar es Salaam , ambako leo hii watamtembelea
Ikulu jijini Kigali
kwa mujibu wa ratiba.
Kagame, ndie amekuwa mfadhili
wa michuano hiyo tangu mwaka 2002, akitoa kiasi cha dola 60,000 kila mwaka kwa
ajili ya zawadi ya mshindi wa kwanza hadi wa tatu.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf
Manji, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba,
wanashukuru kupata mialiko hiyo ya marais na baada ya kurejea kutoka Rwanda ,
watapanga siku ya kwenda kumuona JK kwa pongezi.
Alisema, pamoja na mwaliko
huo, hawana budi kuwashukuru Watanzania kwa michango na hamasa yao , iliyowezesha Yanga
kutwaa ubingwa wa Kagame kwa kishindo, wakiwafunga Azam mabao 2-0.
Kwa ubingwa huo, Yanga imeweka
rekodi ya kuubeba mara tano kama ilivyo kwa AFC Leopards ya Kenya tangu kuasisiwa kwa michuano
hiyo mwaka 1974.
Wakiwa Rwanda , Yanga watacheza mechi tatu
za kirafiki na timu za Rayon, Polisi na nyingine itakayojulikana baadaye.
“Mpaka sasa tunafahamu timu
mbili na hiyo timu nyingine wanashughulikia wenyeji wetu, Chama cha Soka cha
Rwanda (FERWAFA),” alisema Manji.
Aidha, Manji aliongeza kwamba,
beki wao mpya Mbuyi Twite aliyekuwa akikipiga APR, wanatarajia kuungana naye Kigali .