Na Dina
Ismail
KWA muda
mrefu Tanzania tumekuwa wasindikizaji katika michezo mbalimbali na hasa katika
ngazi ya kimataifa.
Licha ya kuwepo kwa wachezaji wengi
wenye vipaji katika michezo husika lakini tumejikuta tukiishia njiani katika
harakati za kusaka tiketi ya kucheza kombe la dunia.
Bahati nzuri tumekuwa tukipata nafasi
za kushiriki katika kuwania kucheza mashindano mbalimbali ya dunia lakini
tumekuwa tukiishia njiani tu na hata tukibahatisha tunatolewa mapema.
Hivi karibuni
timu ya Taifa ya Tenisi kwa watu wenye ulemavu imeweza kuitoa kimasomamso
Tanzania baada ya kufuzu kucheza
mashindano ya kombe la dunia kwa mchezo huo.
Timu hiyo
ilifuzu hatua hiyo bada ya kushika nafasi ya kwanza katika michuano ya Afrika iliyofanyika
Nairobi, Kenya na hivyo itaiwakilisha
Afrika katika mashindano ya Dunia yatakayofanyika nchini Italia mwezi Mei mwaka
huu.
Ni hatua
kubwa na ya kupongezwa kwa timu hiyo pia ni jambo la kujivunia kwani
pamoja na kudaiwa kufanya maandalizi katika mazingira magumu lakini
waliweza kukabiliana na changamoto walizokutana nazo na hatimaye waliweza
kushinda.
Kocha wa
timu hiyo, Riziki Salum alikaririwa na vyombo vya habari akizungumzia
changamoto mbalimbali walizokumbana
nazo katika mashindano hayo lakini
hawakukata tamaa na kuhakikisha wanaitoa kimasomaso Tanzania na Afrika kwa
jumla.
Riziki
alieleza kwamba walikuwa wakifanya mazoezi na maandalizi yao katika mazingira
magumu lakini wachezaji wake waliweza kukabiliana na hali hiyo na kufanya kile
walichodhamiria na matokeo yake waliweza kushinda.
Hivyo basi
ni wakati kwa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia timu hiyo kwa hali na mali
kuhakikisha inafanya vema katika michuano ya kombe la dunia na kuitoa
kimasomaso Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kwamba, jukumu
la kuisaidia timu hiyo lisiachwe kwa viongozi tu wa chama husika bali liwe kwa
kila mwenye nafasi ya kuchangia kufanya hivyo kwani hawa ni wawakilishi wa
Tanzania na si chama binafsi.
Ifikie
wahakati tuachane na kasumba ya kuthamini michezo kama soka au mpira wa kikapu
tu kwa kuipa sapoti kubwa pindi
inaposhiriki mashindano mbalimbali huku michezo mingine ikidharaurika na
wachezaji kuachwa kama watoto yatima.
Fikiria timu
kama hiyo ya watu wenye ulemavu, kwa hali iliyokuwa nayo klakini imeweza kupambana
kadiri ya uwezo wake na kuweza kushinda timu nyingine ambazo zilikuwa na sapoti
kubwa toka kwa wananchi na viongozi wake.
Hiyo ni timu
ya Watanzania wote na itakuwa fahari sana kama itaenda huko na kufanya vema na
kuitangaza vema nchini.
Yaliyopita
si ndwele tuanze sasa kwa timu hiyo na tusisubiri kuja kuipokea na kuandalia
dhifa kubwa, kuialika bungeni au Ikulu
kama itatwaa ubingwa wa dunia wakati walihangaika peke yao katika maandalizi.