VILABU VIWE WAZI KATIKA USAJILI WA WACHEZAJI

Na Dina Ismail
NI kawaida kwa vilabu vya soka ndani na nje ya nchi kufanya usajili kwa ajili ya wachezaji itakoawatumia katika ligi na michuano mbalimbali.
Mara nyingi usajili hufanywa mara mbili, yaani kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi na kabla ya kuanza kwa  raundi ya pili ya ligi.
Kwa vipindi hivyo tumekuwa tukisikia tetesi ama kauli za wazi kutoka kwa viongozi wa vilabu husika kuhusiana na wachezaji wanaosajiliwa ama kuachwa katika vilabu husika.
Kwa Tanzania bado tuko nyuma katika suala la usajili na zoezi hilo hufanywa kisiasa, kisanii na kibabe zaidi kitu ambacho sio kizuri katika maendeleo ya soka letu.
Kwamba, kipindi cha usajili kinapofika badala ufanyike usajili wa kitaalam zaidi, unafanyika usajili kwa ajili ya kutimiza wajibu tu.
Hii ina maana kwamba, suala la usajili inabidi lifanywe na mkuu wa benchi la ufundi yaani kocha ambaye hupendekeza majina ya wachezaji au nafasi ambazo zinahitaji kujazwa, pia wachezaji ambao hawahitaji katika timu.Hapo kazi inabaki kwa uongozi kutimiza kile alichikitaka kocha!
Lakini kwa hapa nchini utaratibu huo haufanyiki kwa asilimia kubwa, kinachofanyika hapo ni ujanja ujanja tu, kwani utakuta kila kiongozi anataka mchezaji wake asajiliwe au upande mwingine kuna viongozi wanataka fulani aachwe wakati kocha anamuhitaji kundini.
Sasa huko ni kuingilia uhuru wa kocha kwani mwisho wa siku timu inajikuta inasajili au inabaki na wachezaji ambao si changuo la kocha hivyo timu itakapofanya vibaya, jumba bovu linamuangukia kocha.
Kocha ni mtaalamu hivyo maamuzi yake hayana budi kuheshimiwa, kinyume na hapo timu itajikuta kila mwaka inabadili makocha, pia kutumia fedha nyingi kila msimu kwa ajili ya usajili, hapo hapo kutopata matokeo mazuri.
Suala jingine ambalo vilabu vya Tanzania vinachemsha kwa upande wa usajili ni uwazi katika mchakato wa zoezi hilo, yaani wenzetu waliopiga hatua wako vizuri kwa kutangaza wazi nyota ambao haitawahitaji baada ya kuisha kwa msimu.
Kutangaza nyota unaowatema mapema ni jambo zuri kwani utatoa nafasi kwa mchezaji kuwa na utayari wa kujijua kwamba hatokuwa katika kikosi hicho hivyo aanze mchakato wa kusaka timu.
Pia kutanngaza mapema wachezaji unaowaacha kutatoa fursa kwa timu nyingine pia kufanya nao mazungumzo kwa ajili ya kuwasajili kwa sababu sio wachezaji wote wanaotemwa ni wabovu!
Lakini cha kushangaza, suala la usajili hufanywa siri sana na hasa wachezaji wanaoachwa na mwisho wa siku zoezi linapofungwa wachezaji walioachwa kujikuta hawana kazi tena kwa msimu mzima.
Kwamba, kipindi cha usajili kimefungwa na klabu ndio inatangaza kuwa imemuacha fulani,sasa hapo unakuwa umempotezea mwelekeo wake sababu mpira ni ajira yake hivyo itabidi aishi maisha ya kubangaiza mpka msimu mpya wa ligi.
Nadhani ifikie wakati kwa vilabu kubadilika kwa kufanya usajili kulingana na Sayansi na Teknolojia.


Post a Comment

Previous Post Next Post