Mwandishi Wetu, Tanga
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani amesema atahakikisha mbio zilizoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania, TASWA za TASWA Mwambao Marathoni zinafanyika kwa kiwango cha juu.
TASWA imeandaa mbio hizo mkoani Tanga zitakazofanyikia Septemba 29, 2024 zikiwa na lengo la kuhamasisha wanamichezo na Watanzania kwa ujumla kutumia Nishati Safi.
Akizungumza baada ya kupokea andiko la Taswa kuhusu mbio hizo, Dk Buriani ameelezea furaha yake kwani haijawahi kutokea kitu kama hicho mkoani Tanga.
Amesema atahakikisha mbio hizo zitakazokuwa za kilomita 21, 10 na kilomita tano zinafanikiwa kwani ni sehemu ya kuutangaza mkoa wa Tanga.
Mbali na kuhamasisha wanamichezo kutumia nishati safi, pia mbio hizo zinahamasisha utunzaji wa mazingira ya Mwambao wa Tanga na kulinda misitu.
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kampeni maalumu kuhakikisha Watanzania na dunia kila mmoja anatumia nishati safi hadi kufikia 2030 ili kulinda afya za wapishi.
Naye Mratibu wa mbio hizo mkoa wa Tanga, Mashaka Mhando amemshukuru Dk Buriani kwa ahadi yake hiyo na kusema mbio hizo zitasaidia kuunadi mkoa wa Tanga ikiwemo hamasa ya matumizi ya nishati safi.