Na Dina
Ismail
MIAKA ya
nyuma Tanzania ilipata kuwa na wachezaji wazuri sana ambao walidumu kwa muda
mrefu katika mpira miguu na baada ya kustaafu walijiendeleza na kuwa makocha.
Ubora na
viwango walivyokuwa navyo ndio vinapelekea sasa hivi kujivunia makocha kama Charles Boniface Mkwasa, Fred Felix Minziro,
Juma Mwambusi, Abdallah ‘King’ Kibaden, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ Salum Madadi,
Sunday Kayuni na wengineo.
Hawa kwa
nyakati tofauti wamepata kuwa makocha wakuu wa timu kubwa kama vile Simba na
Yanga, sambamba na kushika nyadhifa za juu za uongozi wa soka.
Kama hiyo
haitoshi, wakongwe hao wamepata kuwa makocha wakuu ama wasaidizi katika timu za
Taifa kwa nyakati tofauti katika miaka ya hivi karibuni.
Licha ya
kuwepo kwa vipaji vingi hapa nchini lakini ukiangalia kwa haraka haraka kuna
dalili ya kukosekana kwa makocha bora kama hawa katika miaka michache ijayo iwapo
jambo hilo halitafanyiwa hamasa.
Kwamba,
katika miaka ya hivi karibuni wachezaji wengi wazuri baada ya kustaafu waliamua
kuachana na soka na kujikitika katika shughuli zao binafsi.Soka wanacheza tu
kama ni sehemu ya mazoezi yao ya kawaida.
Wakali
waliostaafu mwishioni mwa miaka ya 1990 mpaka 2010 ambao wamechukua kozi za
ngazi mbalimbali za ukocha kama Mohammed
Mwameja, George Masatu, Ali Mayay, Mohammed
Hussein ‘Mmachinga’, Peter Manyika, Boniface Pawasa, Mussa mgosi, Nico
Nyagawa na wengineo kama wangejikita katika ufundishaji naamini tungekuwa
mbali.
Hawa
walikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya timu zao hivyo naamini kama wangegeukia
katika ukocha wangeweza kuzalisha na kuendeleza vipaji vya vijana wanaoibuka kila kukicha.
Hongera kwa
kina Suleiman Matola na Mecky Mexime
ambao hawakutaka kuwa mchoyo wa kipaji vyao
kwa kujiendeleza na taratibu walianza kuonesha mafanikio baada tu ya kustaafu
kwa kuanza kufundisha timu zao.
Matola
ambaye alipata kuichezea Simba na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa nyakati
tofauti, baada ya kustaafu alianzia kocha wa timu ya vijana ya Simba na kuiwezesha
kutwaa ubingwa wa kombe la Uhai,
unaoshirikisha timu za vijana za Ligi Kuu Bara.
Matola pia
ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Ndanda Fc ya Mtwara, pia alipata kuwa kocha
msaidizi wa Simba, huku pia aliwahi
kuifundisha Geita Gold iliyokuwa daraja la kwanza, hivyo akiendeleza juhudi
zake atakuwa mmoja wa makocha bora zaidi katika miaka ya baadaye.
Kwa upande
wa Mexime ambaye alipata kuichezea Mtibwa Sugar na Taifa Stars, baada ya kustaafu
aligeukia ukocha ambako alianza kama kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar na baadaye
kuwa kocha Mkuu.
Mexime kwa
sasa ni kocha wa timu mwenza na Mtibwa, Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Soka
Tanzania Bara.
Tukirejea
katika harakati za wachezaji wa zamani, bado ni kiza kinene kwani hata baadhi
ya wanaojaribu kujiendeleza katika suala la ufundishaji bado hawajawa makini au
kuamua kuwa makocha .
Kwamba,
wengi wanasoma kwa ajili ya kupata vyeti
ili wapate kufundisha timu za mitaani na
zile za madaraja ya chini kitu ambacho hakiwezi kusaidia sana maendeleo
ya soka.
Ingekuwa
vema wakaiga mfano wa kina Mkwassa, Matola na Julio ili miaka ijayo tupate kuwa
na watu wa kujivunia na pia kusaidia
kupunguza kasumba ya timu kuajiri makocha kutoka nje ya nchi.
Pia kwa hali
iliyopo sasa hivi ambako wachezaji wengi vijana ambao hutamba sana na kutokana
na umahiri wao lakini hupotea mapema katika medani hivyo kutishia kuwepo kwa
hazina ya makocha kwa miaka ya baadaye.
Njia
nyingine pia ya kuchangia maendelea ya soka ni kuanzisha vituo endelevu vya
kuzalisha na kukuza soka la vijana hapa
nchini.
Na hiyo
itawahusu hata wale wasiopenda au kuwa
na mwamko wa ukocha kuchangia kwa namna moja ama nyingine ukuzaji wa soka.