TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kumekuwepo na taarifa tofauti kuhusu kuanza kwa Ligi Kuu ya
Bara ambayo kwa mujibu wa kalenda ya Shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
inatakiwa kuanza Septemba 01, 2012. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF na
viongozi wa klabu za Ligi Kuu kilichofanyika Jumatatu ya Agosti 20, 2012 kwenye
ofisi za TFF, TFF inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1. Baada ya kikao
cha pamoja baina ya TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu,
ilionekana kuwa kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya
Ligi na mdhamini wa sasa, yaani Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa
Septemba 15, 2012. Hii inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo
baina ya pande husika, ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.
2. Mazungumzo baina
ya TFF/Kamati ya Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii
kwa kuwa yameshafikia hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza kusainiwa wakati
wowote baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
3. Kukamilika kwa mazungumzo
hayo ni muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila ya matatizo yoyote kwa
klabu zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi
ya mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi;
yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda
muafaka na masuala mengine muhimu.
4. Ratiba ya Ligi
Kuu sasa inatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya
kuanza kwa Ligi Kuu.
5. Kutokana na
kusogwezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii
baina ya mabingwa wa Tanzania Bara na washindi wa pili, nao sasa utapangiwa
tarehe nyingine ambayo ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu. Kwa maana
hiyo mchezo huo utachezwa katika siku itakayotangazwa baadaye.
6. Kuhusu chombo
kitakachoongoza Ligi Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa
Kamati ya Ligi na baadaye kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu kuhusu muundo wa
chombo hicho kulingana na mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la
Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) na Katiba ya TFF na suala hilo kwa sasa
linajadiliwa na klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya hatua za mwisho.
Imetolewa Agosti 21, 2012 na
Angetile Osiah
Katibu Mkuu wa TFF