Simba Sports Club imesikitishwa na hatua
ya Katibu Mkuu wa TFF kujichukulia mamlaka ya Kamati ya Katiba na Sheria na
kuamua mustakabari wa suala la Kelvin Yondani kwa barua yenye kumb namba
TFF/TECH/GC.12/62 ikijibu pingamizi la Simba Sports Club lililokuwa likitaka
mgogoro huo uamuliwe na chombo husika.
Masikitiko hayo ya Simba Sports Club yanatokana
na jinsi haki na misingi bora ya
uendeshaji wa mpira inavyoonekana kupindishwa waziwazi kwani Simba Sports Club
imeshaandika barua nyingine mbili kwa Rais Tenga moja ya terehe 7/6/2012 yenye
Kumb na SSC/5/6/02 ikilalamika juu ya uendeshwaji wa sakata zima la udanganyifu
wa usajili wa mchezaji wa Simba Kelvin Yondani ambayo Rais alitoa maagizo kwa
Katibu Mkuu na nakala kuja kwa Simba SC kwa barua pepe ya tarehe 8/6/2012
lakini baada ya kutofanyika utekelezaji wowote na badala yake watendaji wa TFF
kuendelea kuongea katika vyombo vya habari wakisema mchezaji huyo ni mchezaji
huru, Simba Sports Club iliandika barua nyingine kwa Rais Tenga juu ya kukosa
imani na sekretarieti ya TFF kwa barua
ya tarehe 23/6/2012 yenye kumb na. SSC/24/6/02 jambo ambalo limeonekana wazi
kwamba sekretarieti ya TFF haitendi haki kwa Simba kwa jinsi ambavyo haikufanyia kazi barua mbili lakini
Katibu Mkuu wa TFF amekuwa mwepesi wa kujibu pingamizi wakati si kazi yake ili
mradi timu yake ya Yanga mabayo yeye ni mwanachama ifanikiwe jambo lake.
Katika barua ya pingamizi dhidi ya
mchezaji Kelvin Yondani kutumiwa na klabu ya Yanga katika michezo ya kirafiki
na ile ya CECAFA ya tarehe 11/7/2012
yenye kumb namba SSC/1/7/02 Simba Sports Club iliomba suala la mchezaji huyo
lipelekwe katika kikao cha kamati ya katiba na sheria ambayo muda wake wa kukaa
bado kwani kamati hiyo inaweza kukaa baada ya wiki mbili za kufunga usajili na
kupokea pingamizi mbalimbali lakini taarifa za uhakika ni kwamba kamati hiyo
ilijaribu kuitishwa haraka haraka ili kulitolea suala hili uamuzi lakini corum
haikutimia hivyo ikashindwa kutoa maamuzi lakini kwa ubabe Katibu Mkuu akaamua kujichukulia
mamlaka yasiyokuwa yake na kumpa leseni ya Yanga Kelvin Yondani huku Simba
ikipokea majibu tarehe 14/7/2012 kwa barua uwanja wa Taifa wakati mechi kati ya
Yanga na Atletico imeshaanza na ipo dakika ya 18.
Katika barua yake ya kumuidhinisha Kelvin
Yondani katibu mkuu kakiri kuwepo kwa mkataba wa Yondani na Simba unaoisha mei
31, 2012 na kakiri pia kupokea nyaraka ya makubaliano ya Simba SC na Kelvin
Yondani lakini kwa sababu yeye si mwanasheria na ndio maana kazi hiyo ni ya
kamati ya katiba na sheria amezitafsilia pande mbili za mkataba yaani Simba
Sports Club na Kelvin Yondani nia yao wakati wanaingia mkataba kwamba mkataba
utaanza tarehe 23 december 2012 na kuweka kiambatanisho cha sehemu ya kusaini ya
Simba Sports Club ambayo kwa sababu za kibinadamu ilikosewa na inasomeka tarehe
23 december 2012.
Katibu Mkuu wa TFF ameshindwa/amejikataza
kuusoma mkataba tangu mwanzo na kuona nia za pande za mkataba ni zipi kwani
katika ukurasa wa kwanza mkataba unasoma kwamba umesainiwa tarehe 23/12/2011,
pia mkataba unatambua uwepo wa mkataba wa pande hizo mbili unaoisha tarehe
31/5/2012 na pande husika katika mkataba zimeonyesha nia ya kuongeza mkataba
mara tu ule wa awali unapoisha.
Katika kipengele cha kwanza mkataba
umeshuhudia pande zikitamka waziwazi kwamba mkataba umeongezwa kuanzia
(effective) tarehe 1/6/2012 mara tu mkataba wa awali unapoisha sasa inashangaza
Katibu Mkuu anazitafsilia pande nia zao kwamba mkataba utaanza tarehe
23/12/2012 wakati mkataba umetamka waziwazi.
Pia sehemu aliposaini mchezaji Kelvin
Yondani imeonyeshwa waziwazi kwamba kasaini tarehe 23/12/2011 hivyo kuacha
hitimisho lisilo na shaka kwamba Katibu Mkuu wa TFF amekiuka na kujivika
mamlaka yasiyo yake ili kutekeleza unazi wake wa Yanga.
Simba Sports Club inakusudia kuyakatia
rufaa maamuzi haya ya Katibu Mkuu wa TFF na ipo
tayari kufuata mikondo yote ya sheria mpaka haki ipatikane kwani
itatumia taasisi za TFF kwanza na isiporidhishwa na maamuzi itapeleka suala
hili CAF mpaka FIFA na jambo la kushukuru ni kwamba Shirikisho la TFF limeanza
kujibu barua za Simba SC suala ambalo linaanza kutoa mwanga wa nia ya kutotenda
haki lakini barua hizo zitasaidia kuwaonyesha watu wa nje kama tukifika huko
jinsi mpira wa Tanzania unavyoendeshwa kinazi na viongozi wa Shirikisho.
Imetolewa na
Simba Sports Club