YANGA WAPIGWA 2-0 KAGAME

Atletico wakishangilia bao la pili

MABAO mawili ya Olivier Ndikumana katika dakika ya 81 na 90+3, jana yaliipa Atletico FC ushindi wa 2-0 dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga jana ilicheza ovyo na ilizidiwa katika kila idara- angalau baada ya kufungwa bao la kwanza walijaribu kushambulia kwa mipira ya pembeni, lakini walipopigwa la pili katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90 za mchezo huo ‘walitepeta kabisa’.

Katika mechi ya kwanza ya kundi hilo, APR ya Rwanda iliitandika 7-0 Waw Salam ya Sudan Kusini.

Baada ya mechi hiyo, kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alisema kwamba Atletico ni timu nzuri na  na walicheza vizuri, lakini timu yake haikuwa vizuri leo. Aidha, alisema alipokuja Yanga aliambiwa timu hiyo inacheza mpira wa kukimbiza, ambao yeye hakuutaka.

"Nataka wacheze soka ya utulivu, lakini leo mambo hayakuwa mazuri, taratibu timu itaendelea kuimarika na bado nina matumaini ya kufanya vizuri,"alisema.

Lakini kocha wa Atletico, Kaze Cedric aliiponda safu ya ulinzi ya Yanga, kwamba ilikuwa butu. "Niliiogopa Yanga, nilijua ina wachezaji wazuri, tulijua tutapata upinzani mkubwa, lakini nashukuru tumeshinda. Tulijua Yanga wana kasi, tukaanza kwa kuwatuliza,"alisema Kaze.

1 Comments

  1. Yanga kazeni buti mmetusononesha sana watanzania ukizingatia nyie ni mabingwa watetezi mmeonesha kupwaya sana na hamna maanalizi ya kutosha.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post