Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Airtel Tanzania Jackson Mmbando(kulia)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza kikosi cha timu ya Airtel Rising Stars kinachokwenda kushiriki michuano ya Inter-continental itakayofanyika Nairobi, Kenya baadaye mwezi huu. KAtikati ni Afisa Habari wa kampuni hiyo Jane Matinde na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam(DRFA).
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Wachezaji hao walichaguliwa na jopo la makocha kwa kushirikiana na shirikisho la mpira TFF na chama cha mpira cha Dar es Saalam
DRFA wakati wa fainali za Taifa za Airtel Rising Stars
zilizofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam mwezi
Juni na kushirikisha timu kutoka mikoa ya Lindi, Mbeya, Arusha,
Ilala, Temeke
na Kinondoni.
Akiongea na waandishi wa habari katika ofisi za TFF leo,
Afisa Maendeleo wa mpira wa miguu nchini Salum Madadi aliwataja
vijana watakaowakilisha Tanzania kuwa ni Denis Richard, Juma Hamza,
Abdul Selemani, Ishaka Shekolowa na Bakari Ally kutoka mkoa wa
kisoka wa Temeke.
Wengine ni Abdulatif Mohamed, George Joseph na Badilu Said
(Lindi), Said Kassim, Amos Ikungula, Paul Balama na Goodluck Mabiku
(Ilala),Joel Kasimula na Ibrahim Mtenga (Mbeya), Sntkony Angelo na
Suleiman Yunus (Arusha).
Mashindano hayo yanayotarajiwa kuwa na ushindani mkali
yatashirikisha wachezaji wengine nyota wa ARS kutoka nchi za Kenya, Uganda,
Malawi, DRC, Congo Brazzaville, Nigeria, Ghana, Zambia, Niger,
Gabon, Burkina Fasso, Sierra Leone, Chad, Madagascar na Tanzania.
Mkurugenzi wa mawasiliano wa Airtel Tanzania Beatrice
Singano Mallya amesema kuwa lengo la mashindano hayo ya kimataifa ni kuwapa
vijana fursa zaidi ya kuendeleza vipaji vyao na kupata uzoefu.
"Vile vile Airtel Rising Stars inatoa nafasi kwa wanasoka hawa
chipukizi kuweza kupanua jiografia yao na kujenga urafiki na vijana wenzao
kutoka nchi mbali mbali", alisema Singano.
Michuano hiyo itafuatiwa na kliniki ya soka ya kimataifa
ambayo pia itafanyika Nairobi chini ya walimu wa soka la vijana kutoka
klabu maarufu duniani ya Manchester United ya Uingereza.
Kliniki
kama hii ilifanyika mwaka jana kwenye uwanja wa kisasa wa soka jijini
Dar es Salaam na kushirikisha vijana kutoka Kenya, Malawi, Sierra
Leone na wenyeji Tanzania.
Katika kliniki ya mwaka huu, Tanzania itawakilishwa na
wachezaji sita miongoni mwao ni wavulana watatu na wasichana watatu ambao
walioibuka kuwa wachezaji bora wakati wa fainali za Taifa jijini Dar es
Salaam mwezi Juni.
Airtel Rising Stars ni mpango kabambe wa kuibua na kukuza
vipaji vya wanasoka wanaochipukia barani Afrika.
Walengwa ni wavulana
na wasichana wenye umri chini ya miaka kumi na saba ambao
watapata fursa ya pekee ya kuonyesha vipaji vyao mbele ya waatalum wa mpira
wa miguu wa kitaifa na kimataifa.