MWANACHAMA maarufu wa klabu ya Simba, Zakaria Hanspope
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba, ‘Firend of Simba’
akichukua nafasi ya Salum Abdallah ‘Try Again’ aliyeliongoza kundi hilo kwa
zaidi ya miaka mitano.
Hanspope, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Simba, alichaguliwa katika kikao kilichofanyika juzi, katika hoteli ya JB
Delmonte iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Hanspope alisema,
atajitahidi kufanya kila awezalo, kuhakikisha kundi hilo linafanya kazi kazi
kwa kushirikiana na uongozi, kwa lengo la kuleta maelewano yatakayoijenga Simba
imara na kuleta burudani kwa wapenzi na mashabiki.
“Sisi ni Marafiki wa Simba, tunachokifanya lazima kiendane
na tafsiri ya neno lenyewe na isije ikawa tofauti, kuwa ni maadui wa Simba,
naomba ushirikiano wa pamoja kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,” alisema
Hanspope.
Mbali na Hanspope, wengine waliochaguliwa ni Adam Mgoy
(Makamu Mwenyekiti), Mulamu Ng’hambi (Katibu Mkuu), Katibu msaidizi ni Niki
Magariza huku Juma Pinto ni msemaji wa kundi hilo.
Awali, mmoja wa waasisi wa kundi hilo, Jaji mstaafu Thomas
Mihayo, alisema mwelekeo na dira ya kundi hilo lilipotea, hivyo kuwa na imani
kwa viongozi wapya kufanya kazi ambayo itakuwa na faida kwa maendeleo ya Simba.
Jaji Mihayo alisema, kundi hilo limekuwa na malengo mazuri,
lakini kinachokwamisha sasa hivi ni wanachama wake kutokuwa wamoja na kuwataka
kurudisha umoja na kufuatialia mambo ambayo yanapangwa kwa ajili ya
utekelezaji.
Mbali ya Salim ambaye katika uongozi wake alileta mafanikio
makubwa ndani ya klabu ya Simba, kwa uhamasishaji wa kundi hilo lilijizolea
umaarufu mkubwa ndani ya klabu hiyo, viongozi wenginge wa zamani ni Johnson
Masabala (Makamu Mwenyekiti), na Issa Batenga aliyekuwa katibu wa kundi hilo.