UONGOZI wa klabu ya Moro United umeweka mikakati ya
kuhakikisha timu hiyo inashiriki vema ligi daraja la kwanza na hatimaye kurejea
tena katika ligi kuu soka Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa timu
hiyo Rodgers Peter alisema kwamba katika kuhakikisha hilo linatimia wameona
waziungatie zaidi katika kusajili kikosi ambacho kitashiriki kikamilifu ligi hiyo
itakayoshirikisha timu 24.
Alisema usajili wao umezingatia wachezaji chipukizi zaidi na
wenye vipaji vya hali ya juu hali itakayowafanya waweze kukaa kwa muda mrefu na
hivyo kuifanya timu kuwa na umoja.
“Yaani tumedhamiria kurejea katika ligi kuu bara,
tumehakikisa tunasajili wachezaji chipukizi ili tuwe nao kwa muda mrefu na timu
iweze kucheza kitimu hasa, pia tumeangalia kipaji binafsi na uwezo wa kuhimili
mikiki mikiki ya uwanjani”, alisema Rodgers.
Rodgers aliongeza kuwa, kikosi cha timu hiyo kinaendelea na
mazoezi yake ya kujiandaa na ligi hiyo katikia uwanja wa Kwa Bibi uliopo Tabata
Segerea chini ya kocha wake Mkuu, Yussuf Macho ‘Musso’.
Alisema, pamoja na mazoezi yake timu yake inacheza mechi
mbalimbali za kirafiki ambazo zinamsaidia kocha wao kujua kiwango cha wachezaji
wake na kama kuna mapungufu ili aweze kuyafanyia marekebisho kabla ya kuanza
kwa ligi hiyo.