Hapa ndipo gundu lilipoanzia; Mudde akikwatuliwa na wachezaji wa Express na kusababisha maumivu ambayo leo yanamponza kutemwa Simba. (Habari picha kwa hisani ya bongostaz.blogspot.com) |
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema jioni hii kwamba, Mudde atakuwa nje ya Uwanja kwa miezi mitatu hivyo hataweza kucheza kabisa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na kwa sababu hiyo anaondolewa na nafasi yake anapewa Keita.
Tayari Keita yupo na Simba kambini mjini Arusha na ingawa jana katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mathare United, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha aliumia na kutoka nje Wekundu wa Msimbazi wakishinda 2-1, lakini imeelezwa leo alifanya mazoezi na wenzake.
Kwa marekebisho hayo, wachezaji wa kigeni wa Simba SC wanakuwa ni Keita, Emmanuel Okwi kutoka Uganda, Daniel Akuffo kutoka Ghana, Felix Sunzu kutoka Zambia na Paschal Ochieng kutoka Kenya.
Aidha, Mudde anakuwa mchezaji wa kigeni wa tatu kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao na kutemwa kabla ya kuanza kazi, wengine wakiwa ni Lino Masombo na Kanu Mbivayanga, wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).