Mwenyekiti wa Tanzania Women of Achievement (TWA) Ms. Irene Kiwia akitoa mada kwenye semina ya Kinara.
Muelimishaji rika Bi. Suzanne Mrema akiongea na wasichana.
Kampeni ya Kinara ni Mimi Jasiri ina lengo la kuelimisha mtoto wa kike aweze kujitambua na kujijengea uwezo yeye mwenyewe kupambana na mambo mbalimbali yaliyomzunguka kwenye jamii,jinsi gani ya kuepuka mimba za utotoni,kuhakikisha mtoto wa kike anasoma na kupambana na imani potofu zinazowakabili miongoni mwa jamii zetu.
Kampeni hizi zitaanzia mikoa ya Dar es Salaam,Lindi, Mtwara na Iringa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wasichana wanaopata mimba za utotoni na kupelekea kuacha shule.
Kwa kuanzia, kampeni zimeanza kata ya kimara zimekutanisha vitongoji vyote vya Kata hiyo ambapo idadi ya wasichana waliojitokeza walikuwa mia tatu (300) kati yao wakiwa ambao wameacha masomo kutokana na sababu mbalimbali na wale ambao wanaendelea na masomo.
Balozi wa Kinara Ni Mimi Jasiri Dkt. Marina Njelekela Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambaye ni mshindi wa tuzo za wanawake wenye mafanikio Tanzania 2011 alifungua semina na kuwahasa wasichana kujikita kwenye kufanikisha malengo yao na kuepukana na mimba za utotoni, kujiepusha na tabia na mazingira hatarishi yanayoweza kuwakatishia masomo yao au kuwaharibia maisha yao hususani magonjwa kama HIV/AIDS na kuachana na imani potofu.
Semina ilihusishwa wawezeshaji mbalimbali ambao waliongelea mada muhimu kama kujitambua, malengo na jinsi ya kuyatimiza, muonekano na mazingira, haki za watoto na wanawake, HIV/AIDS na elimu ya jinsia. Miongoni mwa wawezeshaji alikuwepo Bi. Sadaka Gandi-Mwanasaikolojia na Kansela mahiri, na Bi. Suzie -Mshahuri nasaha wa mambo ya kijamii na mwelimishaji rika. Wasichana pia walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kutoa maoni yao.
Naye mwenyekiti wa Tanzania Women Of Achievement(TWA) Bi. Irene Kiwia aliwahasa wasichana kujijengea uwezo wa kujitambua na kujiamini, akisisitiza kuwa msichana akijua uwezo mkubwa alionao kufanikiwa kimaisha atajitunza, atajipanga na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo yake makubwa. Aliwahimiza wasichana kuwa wana nafasi kubwa sana kwenye jamii zinazowazunguka, ni jukumu na wajibu wao kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii na kufanya kazi kwa bidii ili wawe vinara wa kuigwa kwenye jamii.