Na Mwandishi Maalumu, Gaborone
MSHAMBULIAJI
wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Mrisho Ngassa, ameacha gumzo jijini hapa baada
ya kuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Botswana ‘Zebras’ katika moja kati ya
mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA),
zilizochezwa juzi, siku.
Katika
pambano hilo , Ngassa
alifanikiwa kuiongoza Stars kupata matokeo ya sare ya mabao 3-3 katika mechi ya
kimataifa ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Molopolole.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilikuwa ikishangiliwa na
watanzania zaidi ya 100 wanaoishi nchini Botswana , huku wakiwa na bendera ya
Taifa.
Mashabiki
wa soka mjini hapa, walianza kulitambua jina la Ngassa baada ya kufanikiwa
kuwatoka mabeki wa Zebras, kabla ya kipa wa timu hiyo Mompolok Sephekolo
kumchezea rafu ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru ipigwe penalti,
iliyofungwa kwa ustadi mkubwa na beki Erasto Nyoni dakika ya 18.
Baada
ya bao hilo , Botswana
walianza kulishambulia lango la Stars kama
nyuki na dakika ya 25, mshambuliaji
Lemponye Tshireletjo alisawazisha, baada ya mabeki wa Stars kushindwa kuokoa
mpira uliopigwa kutoka upande wa kushoto na kumkuta aliyeunganisha mpira wavuni,
huku kipa Juma Kaseja akishindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Hata
hivyo, baada ya wanyeji kupata bao la kusawazisha, kiungo Mwinyi Kazimoto
akaifungia Stars bao la pili dakika ya 31 kwa shuti kali la mita takribani 30.
Kazimoto,
alifunga bao hilo
baada kipa wa Zebras, Sephekolo kushindwa kudaka shuti la Ngassa alilookoa kwa
mguu na mpira kumkuta mfungaji.
Mbali
ya kazi kubwa iliyokuwa ikifanywa na Ngassa kwa kushirikiana vizuri na Haruna
Moshi ‘Boban’ pamoja na Said Bahanuzi na kufunikiwa kucheka na nyavu, safu ya
ulinzi iliruhusu mabao kuingia nyavuni kirahisi.
Hali
hiyo, iliendelea dakika ya 37 ikiwa ni dakika 6 tu tangu Kazimoto alipofunga
bao la kuongoza, mshambuliaji mahiri wa Zebras, Tshireletjo alipachika bao lake
la pili na la kusawazisha, baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa
kutoka pembeni mwa
uwanja
na kumshinda Kaseja na kufanya matokeo kuwa 2-2 hadi kipindi cha kwanza
kinamalizika.
Kipindi
cha pili, timu zote ziliingia uwanjani zikiwa na lengo la kupata mabao ya
kuongoza, huku Botswana
ikiwa ya kwanza kupata bao lililofungwa kwa kichwa tena na Tshireletjo dakika
ya 70.
Stars,
ilipata pigo dakika 80, baada ya beki Erasto Nyoni kulimwa kadi nyekundu baada
ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Botswana , huvyo kumlazimisha Kocha
Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen, kufanya mabadiliko ya kumtoa Boban na Bahanuzi
na nafasi zao kuchukuliwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ na Simon Msuva.
Mabadiliko
hayo yaliongeza uhai kwa Stars huku Msuva akishirikiana vema na Ngasa na katika
dakika ya 90, Msuva alifanya kazi ya kuwatoka mabeki wa Botswana kabla ya kutoa pasi ya
mwisho kwa Ngassa aliyetupia mpira kambani na kubadili matokeo kuwa 3-3.
Akizungumzia
matokeo hayo, Kocha Poulsen alisema kuwa, timu yake ilicheza vizuri isipokuwa
safu ya ulinzi ndio haikufanya kazi yake ipasavyo.
“Nikweli
kabisa kwamba, beki haikucheza vizuri, kwani waliwachosha washambuliaji wangu,
haina maana ya kufunga mabao kisha yanarudi, inatia hasira kuona mabao
yanafungwa kirahisi ndani ya dakika chake, yaani sisi tunafunga mabao ya shida
lakini wao wanafunga mabao mepesi, hivyo nitayafanyia kazi mapungufu hayo kabla
ya mechi inayofuata," alisema Poulsen.
Stars
imerejea jijini jana usiku.