Lloyd Nchunga
Imani Madega
MABINGWA wa Ligi Kuu Bara,
Simba ya jijini Dar es Salaam, wamewasilisha barua Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), wakimpinga Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji
ya Shirikisho hilo, Wakili Alex Mgongolwa, pamoja na wajumbe wake wawili kwa
madai ya kutokuwa na imani nao.
Wajumbe waliopingwa sambamba
na Mgongolwa ni waliowahi kuwa wenyeviti wa klabu ya Yanga, mawakili Lloyd
Nchunga na Iman Mahugila Madega.
Pingamizi hilo la Simba,
linatokana na kutokuwa na imani na viongozi hao katika kuamua suala la usajili
wa wachezaji waliozua utata, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, ambao awali Simba
inadai iliwasajili kabla ya Yanga kuingilia kati na kuwanyakua.
Kamati hiyo ilikuwa ikutane
jana na leo kwa ajili ya kupitia usajili wa klabu za Ligi Kuu Bara na Ligi
Daraja la Kwanza , lakini kutokana na kusogezwa
mbele kwa ligi hiyo, wanatarajiwa kukutana katika tarehe itakayopangwa baadaye.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ alisema
wamewasilisha barua hiyo ili kuomba kushughulikiwa kwa ombi lao kwa hofu ya
kutotendewa haki.
Alisema kuwa Mgongolwa pamoja
na kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, pia amepata kuwa mjumbe wa kamati za Yanga,
huku Madega na Nchunga nao wakiwa ni wanachama waadilifu na waaminifu wa klabu
hiyo, hivyo ni rahisi kuipendelea.
Aliongeza kuwa kutokana na
wajumbe hao wa kamati kuwa na damu ya Yanga, wanaamini hawatatoa maamuzi sahihi
kuhusiana na suala linalohusu utata wa usajili wa wachezaji hao, hivyo TFF
haina budi kutumia busara kuwaondoa.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa
Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, alitangaza kujiuzulu ujumbe wa kamati hiyo,
kabla ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kukutana naye na kumweka sawa, hivyo
kubadili msimamo wake.