WAKATI wingu zito likitanda
juu ya kuja nchini kwa beki Mbuyu Twite, uongozi wa Yanga umeibuka na kudai
atawasili nchini leo na kuwataka mahasimu wao, Simba, wamsubiri na ‘RB’
wanayodai kuikata ili kumkamata.
Beki huyo, ambaye usajili wake
ulizua utata baada ya awali kusaini Simba kwa dola 30,000 za Marekani akipitia
timu ya APR ya Rwanda
inakodaiwa kuwa alikuwa akicheza kwa mkopo, kabla ya Yanga kuzunguka upande wa
pili katika klabu yake ya awali, FC Lupopo ya DRC na kumsainisha kwa dola
50,000.
Kutokana na kusaini Yanga,
Twite alituma wawakilishi warejeshe fedha za Simba jijini Dar es Salaam, lakini
viongozi wa klabu hiyo waligoma na kumtaka azirejeshe mwenyewe, huku pia wakidai
kuwa wamemfungulia jalada polisi na wana ‘RB’ mkononi kwa madai kuwa, mchezaji
huyo amefanya kitendo cha wizi wa kuaminiwa.
Kitendo cha Twite kushindwa
kutua nchini Jumatatu, Agosti 26 na kikosi cha Yanga alichoungana nacho huko
Rwanda kilipokuwa ziarani, kuliibua maneno kuwa beki huyo anagwaya ‘mkwara’ wa
Simba.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine, alisema, Twite atatua
Uwanja wa Kimataifa wa JK Nyerere leo na ndege ya Rwanda Air, majira ya saa
9:30 alasiri na kuwataka Simba wamsubiri na RB yao uwanjani hapo.
Akihojiwa hivi karibuni na
kipindi cha Spoti Leo cha Radio One, baada ya Yanga kurejea ikitoka Kigali,
Rwanda bila Twite, Ofisa Utawala wa Simba, Evodias Mtawala, alisema kuwa, bado wanamsaka
nyota huyo, akidai maelezo ya utapeli aliofanya waliyaripoti Polisi Makao
Makuu.
Lakini alipoulizwa Msemaji wa
Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alishangazwa na madai hayo, kwa maelezo
kuwa, Makao Makuu ya Jeshi hayahusiki na utoaji wa RB, na kwamba viongozi Simba
wanapaswa kuulizwa walikopata kibali hicho.
“Napenda nikuhakikishie ndugu
yangu Makao Makuu ya Polisi hayahusiki na kitu kama
hicho. Watafute Simba wakuambie wapi walikofikisha malalamiko yao na kupewa RB,” alisema huku akiongeza
kuwa wanaweza kufungua na kupata RB kutoka vituo vya polisi na sio makao makuu.