YONDAN AANZA KUJUTA YANGA, AZITAKA HELA ZA TWITE


UKISTAAJABU ya Musa utayaona ya Firauni. Katika hali isiyotarajiwa, beki aliyesajiliwa kwa mbwembwe na mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga, Kelvin Yondani ameanza kujutia uamuzi wake huo na kutaka kurejea klabu yake ya zamani, Simba.
Habari za uhakika zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, zinaeleza kuwa, Yondani tayari amebainisha mawazo yake hayo kwa viongozi wake wa zamani wa Simba, ambao ndio watu wa karibu na wanaomsapoti kwa mambo mengi.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, Yondani amewaambia wadau wake hao wa Simba kuwa, watakaporejeshewa fedha zao dola 30,000 walizompa beki Mbuyi Twite, wampe yeye ili afanikishe kurejea Msimbazi.
Simba ilitangaza kumsajili Twite kwa kitita hicho,
kabla kuzidiwa kete na Yanga, huku beki huyo akituma wawakilishi nchini kurejesha fedha alizochukua awali, jambo ambalo lilikataliwa na Wekundu wa Msimbazi, ambao walimtaka mchezaji huyo azirejeshe mwenyewe.
“Unajua Yondani hivi sasa hajisikii vizuri, kwani hata watu wake hao wa karibu wa Simba wamehuzunishwa sana na uamuzi wake wa kuhamia Yanga, hivyo hata ule ukaribu wa awali umepungua, hivyo kawafuata na kuwataka kurejea,” kilisema chanzo hicho.
Imeelezwa kuwa, katika makubaliano ya Yondani kusajiliwa Yanga, alilipwa sh milioni 15 na kiasi kilichobaki atamaliziwa baadaye, hivyo amekubaliana
na Simba wampe fedha hizo za Twite, ili arejeshe
kiasi alichochukua Jangwani.
Sababu nyingine inayoelezwa Yondani kujuta kusaini Yanga, ni hofu ya kuwepo kwa vita ya namba katika kikosi cha mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati.
Habari hizo zimedokezwa huku suala la usajili wa Yondani likigubikwa na utata mkubwa baada ya Simba na Yanga zote kumsajili kwa ajili ya Ligi Kuu ya Bara.
Tayari sekretarieti ya Shirikisho la Soka Tanzani (TFF), limeagiza Kamati ya Nidhamu, Maadili na Hadhi za Wachezaji, kufanya maamuzi.
Hiyo inatokana na Yondani kujiunga na Yanga kwa kitita cha sh milioni 30 kama mchezaji huru, hoja ambayo inapingwa na Simba, ikisema bado ni wao.
Kwamba, ingawa mkataba wa Yondani ulikuwa ufikie ukomo Mei 31, mwaka huu, lakini Desemba 23, 2011, waliurefusha, ingawa mwaka unasomeka 2012.

1 Comments

  1. taarifa hiyo haina hadhi ya kuwa habari imejichanganya kimaelezo

    ReplyDelete
Previous Post Next Post