KLABU ya soka ya Simba inadaiwa kumteka kwa nguvu beki
wa Yanga, Kelvin Yondan.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kwamba zoezi hilo lilifanyika juzi usiku ambapo mchezaji wa zamani wa
Simba (jina kapuni) aliendesha zoezi hilo kwa lengo la kumlazimisha kurejea
Simba.
Inadaiwa mchezaji huyo wa zamani wa alikwenda nyumbani
kwa Yondan na wakati anaondoka aliomba kuendesha gari ya Yondan aina ya
Mitsubishi Pajero lakini cha kushangaza mkongwe huyo aliendesha gari na mpaka
kwenye ofisi za kiongozi mmoja wa Simba.
“Walipofika huko aliwekewa mil.20 mezani na kutakiwa asaini
fomu za kielektronik (Transfer Match System) na ndipo alipotafuta upenyo wa
kutoka na kumpigia simu mmoja ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga Seif
Ahmed ili kuomba na msaada,”alisema mtoa habari huyo.
Taarifa zinaongeza kwamba, Yondan alipata upenyo wa
kutoka baada ya mwenyeji wao kutoka na kwenda kuwasha gari lake lakini askari
walimzuia kabla ya kudanganya kuwa ametumwa vocha na kiongozi huyo wa Simba na
ndipo aliporuhusiwa na kuondoka.
Baada ya kuchomoka mikoni mwa watu wa Simba, Yondan
alikutana na baadhi ya viongozi wa Yanga na kwenda kituo cha polisi Kilwa na
ndipo walipofungua jalada namba KLR/RB/4774/2012.
Gazeti hili lilimtafuta kiongozi wa Simba anayehusishwa
kwenye sakata hilo ambapo simu yake iliita bila kupokea kabla ya baadaye kuamua
kuizima kabisa.
Hata hivyo, Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga
alisema taarifa hizo ni uzushi mtupu kwani zilikuwa na lengo la kuivuruga
kamati ya Sheria, Maadili nah ADHI za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) kutoa maamuzi yake kuhusiana na suala la mchezaji huyo ambaye Simba
ilimuwekea pingamizi.
Kwa upande wa Yanga kupitia kwa katibu wake, Mwesigwa
Selestine alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa vile tayari limeshafikishwa
katika vyombo vya dola hivyo wanaviachia vifanye kazi yake.
Alipotafutwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Temeke David
Missime alishangazwa na taarifa hizo na kusema ni uzushi usiokuwa na mashiko
ambao alidai ni wa kutafuta umaarufu.
Alisema haiwezekani kumsemea mtu mwenye akili na
ingekuwa na mashiko kama mhusika alitekwa na ameshindwa kupatikana au
alipatikana akiwa hajitambui ndipo wangeweza kufungua jalada lakini si kwa
taarifa za uzushi.