Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika
juzi (Septemba 1 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama
hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KRFA walivyo na imani kubwa
kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Kigoma.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya KRFA chini ya uenyekiti wa Omari Saleh Mkwarulo ambaye amechaguliwa
kwa kipindi cha kwanza.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Kigoma kwa kuzingatia
katiba ya KRFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KRFA na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu
wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Omari
Saleh Mkwarulo (Mwenyekiti), Issa Bukuku (Katibu), Ahmed Msafiri Mgoyi (Mjumbe
wa Mkutano Mkuu TFF) na Mohamed Nassoro (Mwakilishi wa Klabu TFF).
Nafasi za Makamu Mwenyekiti na Katibu Msaidizi zitajazwa
kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye baada ya waliogombea ambao hawakuwa
na wapinzani kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)