MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba,
wanatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo kutokea Arusha walikokuwa
wamepiga kambi maalumu ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara
inayotarajiwa kuanza Septemba 15 mwaka huu.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga,
alisema jana kwamba, mara baada ya kuwasili, wataunganisha kambini moja kwa
moja kuendelea na maandalizi yake ya ligi hiyo na keshokutwa watacheza mechi ya
kujipima ubavu na Sofapaka ya Kenya.
Alisema, wachezaji wote wapo katika
hali nzuri na kupitia kambi ya Arusha, kikosi kimepata maandalizi ya kutosha
yakiambatana na mechi kadhaa za kujipima ubavu, hali ambayo inawapa matumaini
ya kufanya vema katika michezo yake.
“Tunashukuru kambi imekuwa na mafanikio
sana, kwani kikosi chetu kwa sasa ni tishio, hivyo timu zinazoshiriki ligi kuu
bara zikae chonjo kwani tutakuja na moto usio na kipimo,” alisema Kamwaga.
Simba itaanza kuvaana na Azam FC katika
mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 11,
kabla ya kuanza kampeni zake za kutetea taji lake dhidi ya African Lyon,
Septemba 15 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha Simba kinachonolewa na
Mserbia Milovan Cirkovic, juzi kilikwaana na Soni Sugar ya Kenya na kulazimisha
sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.