MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom, Simba
leo wanatarajiwa kuwakabili maafande wa Prisons ya Mbeya katika mechi
itakayochezwa katika Uwanja
wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba, mabingwa watetezi wa ligi hiyo
iliyonza Septemba 15, watashuka dimbani wakitaka kuendeleza rekodi ya
kutofungwa baada ya kushinda mechi zote tatu, hivyo kuwa na piinti 9.
Hesabu za Simba ni kutaka kushinda mechi
ya leo ili kujiweka fiti zaidi kisaikolojia kuikabili Yanga katika mechi ya
aina yake itakayopigwa Oktoba 3, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema
jana kwamba, kikosi cha Simba kipo tayari kwa Mechi ya leo na hakuna kingine
wanachokitaraji kutoka kwa Prisons zaidi ya ushindi kabla ya kugeuzia makali
hayo kwa Yanga.
Kamwaga alisema kwa vile timu hiyo imepiga
kambi Visiwani Zanzibar, itatua jijini Dar es Salaam kwa ndege kisha itarejea huko
baada ya mechi hiyo kuzidi kujipanga kwa ajili ya mechi ya Yanga ya hapo Jumatano.
Alisema kupitia kazi kubwa iliyofanywa
na Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovic hawana shaka timu hiyo itaendeleza
wimbi la ushindi kama walivyofanya kwenye mechi tatu zilizopita tangu kuanza
kwa ligi hiyo.
Kuhusu hali ya kikosi, alisema wapo
katika hali nzuri isipokuwa Haruna Moshi ‘Boban’ anayesumbuliwa na malaria,
hivyo kazi inabaki kwa kocha kupanga nyota wengine watakaoiwezesha kupata
pointi zote tatu.
Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa yenye ushindani
mkubwa kutokana na kila timu kuwa kuonesha uhai tangu kuanza kwa ligi hiyo, itaanza
saa 11 jioni na kurushwa live na kituo cha Televisheni cha SuperSport cha
Afrika Kusini.
“Tunafahamu wapinzani wetu ni moja ya timu bora zinazoshiriki ligi hii
lakini kikubwa ni kwamba tumejipanga vema kukabiliana na timu yoyote kwa
kuhakikisha tunacheza kwa nguvu zote na hatimaye kushinda,”alisema Kamwaga
Simba inawakabili Prosons wakitoka
kuwafunga African Lyon (3-1), JKT Ruvu (2-0)
na Ruvu Shooting mabao 2-1,
hivyo leo watakuwa wakipigania ushindi wa nne mfululizo.