SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF),
limeishukuru Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom kwa kuingia mkataba mpya wa udhamini wa ligi kuu soka tanzania Bara.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema kuwa,
mkataba huo ambao ni mnono na mara mbili zaidi ya ule wa uliopita, anaamini
utazisaidia vilivyo klabu shiriki.
“Ni wazi kuwa, mkataba huu una
maslahi kwa klabu zetu pamoja na soka la Tanzania kwa ujumla, kwa sababu umeongeza
maradufu fedha za udhamini,” alisema Tenga.
Tenga alisema kuwa, kuhusu
wadhamini hao kuondoa nembo kifuani na kuweka mabegani, ni hatua nyingine kubwa
inayotoa fursa ya kuziwezesha klabu kunufaika.
Alisema, kwa sasa klabu
zitaruhusiwa kuweka mabango ya wadhamini wowote watakaowapata, isipokuwa wale
ambao ni washindani wa Vodacom kibiashara.
Aidha, Tenga ameishukuru pia
SuperSport kwa kukubali mwaka huu kuonesha mechi nyingi zaidi ya mwaka jana na
mwaka juzi.
“Hii ni faraja kubwa sana
kwetu, kwa sababu mwaka jana na mwaka juzi SuperSport walionesha mechi za Yanga
na Simba tu,” alisema Tenga.
Tenga alisema kuwa, hilo
litasaidia kulitangaza soka la Tanzania nje ya nchi na kuvuta wawekezaji,
pamoja na wadhamini wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Tenga aliwaomba
wadhamini kujitokeza kudhamini timu ya Taifa ya Wanawake, ‘Twiga Stars’ pamoja
na zile za vijana chini ya miaka 20, U-20 ‘Ngorongoro Heroes’ na U-17 ‘Serengeti
Boys’.
Lakini wakati Tenga
akiipongeza Vodacom, timu kadhaa zinazoshiriki ligi kuu bara, zimekuwa
zikivutana na Shirikisho hilo kwa madai hazinufaiki ipasavyo kutokana na
gharama wanazotumia hivyo kutaka kuruhusiwa kusaka wadhamini wengine ikiwamo
washindani kibiashara na Vodacom.
Katika hatua nyingine,
pambano kati ya Azam FC na JKT litakalopigwa leo Iwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, litaoneshwa ‘live’ na SuperSport kuanzia saa 1:00 jioni.