MCHEZO wa raundi ya kwanza ya ligi kuu soka Tanzania Bara
baina ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga utarushwa ‘Live’ kupitia kituo cha
televisheni cha Super Sport chenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini.
Mechi hiyo ambayo itachezwa Oktoba 3 kwenye uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa mechi tano za ligi hiyo zitakazorushwa
‘live’ na kituo hicho kwa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa habari wa
Shiriukisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura alisema kwamba hatua hiyo
imetokana na kuwepo kwa mazungumzo ya udhamini wa kituo hicho kwa ligi kuu
utakaoanza mwakani.
Alisema kutokana na mazungumzo hayo kutokamilika wameona
waanze kwa majaribio kwa kuonesha mechi hizo tano na mwakani wataendelea na
ratiba nyingine baada ya mipango kukamilika.
“Kama mjuavyo Super Sport wana ratiba zao na mambo mengi
hivyo inabidi kujipanga kwanza, lakini mazungumzo yanakwenda vizuri na ndiyo
maana kwa kuanzia wataonesha mechi hizo tano.
Mbali na mechi hizo, Wambura alisitaja mechi nyingine
zitakazorushwa ‘Live’ na kituo hicho ni pamoja na ule wa Azam Fc dhidi ya JKT
Ruvu utakaochezwa Uwanja wa Chamazi, pamoja na ule wa Simba na Prisons
utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salam ambapo mechi hizo zote zitafanyika
Septemba 28.
Mchezo mwingine ni kati ya Yanga dhidi ta African Lyon
utakaochezwa Septemba 30 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, sambamba
na ule wa Ruvu Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa katika dimba la
Chamazi.
Ligi kuu soka Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi
Septemba 15 mwaka huu chini ya udhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom.