WANACHAMA maarufu wa klabu ya
Simba, Hassan Othman ‘Hassanoo’ na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wamefanikiwa tena
kuukwaa uongozi wa chama cha soka mkoa wa Pwani (Corefa).
Katika uchaguzi huo
uliofanyika Wilaya ya Mafia mkoani Pwani jana, Hassanoo alifanikiwa kutetea
nafasi yake ya uenyekiti ambaye katika uchaguzi huo hakuwa na mpinzani ambapo
alizoa kura zote 22.
Aidha,Kaburu ambaye ni makamu
Mwenyekiti wa Simba, naye aliweza kutetea nafasi yake ya ujumbe wa Mkutano Mkuu
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kuzoa kura zote 22 za wajumbe
walioshiriki kupiga kura.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi
ya Corefa, Masau Bwire alisema jana kwamba viongozi hao wapya watakiongoza
chama hicho kwa miaka minne, amapo kwa upande nafasi ya Katibu Mkuu ilikwenda
kwa Riziki Majala ambaye alipata kura 20 za ndiyo na mbili za hapana.
Alisema nafasi ya Katibu
Msaidizi ilikwenda kwa Mohamed Lubondo aliyepata kura 22, huku Abubakar Allawi
aliukwaa Uhazini kwa kura 22, wakati Juma Kisoma alishinda nafasi ya Uwakilishi
wa Vilabu (TFF) kwa kura 14 na nafasi ya Mwakilishi kwa upande wa Wanawake
ilikwenda kwa Florence Ambonisye aliyezoa kura zote 22.
Bwire aliwataja wajumbe
waliochaguliwa katika kamati ya utendaji ambao wote walizoa kura 22 za ndiyo ni
pamoja na Godfrey Haule, Musa Bakari na Gwamaka Mlagila.