Mwamuzi, Mathew Akrama katikati
Kamati ya Ligi imewaondoa waamuzi watatu wa Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kwa kushindwa kumudu michezo waliyopangiwa. Waamuzi hao ni Mathew
Akrama wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 80 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati
ya Yanga na Simba iliyochezwa Oktoba 3 mwaka huu.
Wengine ni Paul Soleji wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya
Simba na Tanzania Prisons, na mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo
Mwarabu Mumbi wa Morogoro. Pia mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga
na Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam amepewa onyo.
Kamishna wa mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon,
Pius Mashera ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa
kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na uwanjani.
Vilevile Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko
dhidi ya msimamizi wa kituo cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la
kinidhamu ametakiwa alipeleke kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
Nayo Simba imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa
kuchelewa kufika kwenye pre match meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons
(sh. 100,000) na kwa washabiki wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi
hiyo (500,000).
Pia Kamati ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa
Shabani Kado wa Mtibwa Sugar kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting
mara baada ya mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la
kinidhamu lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.