Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Bi. Kushilla Thomas akishirikiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Bi. Juliana Yassoda kukata utepe kuzindua rasmi mbio za Kilimanjaro Marathon 2013 zinazotarajiwa kufanyika Moshi mwezi Machi mwaka 2013. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki. (Picha: Executive Solutions)
PRESS RELEASE
Mbio za 11 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa
kufanyika tarehe 3 Machi 2013 huko Moshi zimezinduliwa.
Akiongea kwenye uzinduzi huo jijini Dar es salaam,
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Bi. Kushilla Thomas
alisema bia ya Kilimanjaro Premium Lager inaendelea na udhamini wa mbio hizo
zinazoendelea kuwa kubwa na bora kila mwaka huku zikiibua vipaji vipya na
kuwapa wanariadha chipukizi fursa ya kukua na kuweza kushindana kimataifa.
“Kilimanjaro Premium Lager inalenga kuendeleza riadha
kwa kukuza vipaji, kuwapa wanariadha wetu jukwaa la kushindania na wanariadha
kutoka mataifa mbalimbali.” Alisema Kushilla.
Aliongeza kuwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ina
lengo la kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa na mvuto kwa wanariadha wenye
vipaji ili kuongeza ubora wa riadha ya Tanzania ili Watanzania waweze kushiriki
kikamilifu kwenye mashindano makubwa duniani.
Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium
Lager, George Kavishe alisema: “Kupata washiriki kutoka nchi mbalimbali
inatusaidia kuonyesha dunia kuwa Kilimanjaro Marathon nini lakini kuwaendeleza
na kuwapa moyo wanariadha Watanzania ni kipaumbele chetu kikubwa, kwa sababu
hiyo tumeanzisha zawadi maalum ya shilingi milioni 3 kwa Watanzania
watakaomaliza wakiwa wa kwanza katika mbio za 42km Kilimanjaro Premium Lager
Marathon na hii ni mbali na zawadi watayopata kwa nafasi watakazoshinda.”
“Maandalizi ya Kilimanjaro Marathon 2013 yameishaanza
ili kuhakikisha mbio hizo zinakuwa bora kama ilivyo utamaduni wetu kuhakikisha
tunaboresha kila mwaka ili kuwapa raha ya aina yake washiriki pamoja na
watazamaji.”
“Kwa mara
nyingine tena, Kilimanjaro Premium Lager itaendelea kuwathamini wanariadha kwa
kuwatunuku zawadi nzuri ya fedha taslimu huku ikiwapa watazamaji burudani ya
aina yake.”
Zawadi ya fedha taslimu kwa washindi wa kwanza hadi wa
tatu wanaume kwa wanawake kwenye mbio ndefu za km 42.195 zijulikanazo kama
Kilimanjaro Premium Lager Marathon itakuwa ni shilingi milioni 3 , washindi wa
pili watajipatia shilingi milioni 1.5 kila mmoja huku washindi wa tatu
wakijipatia shilingi 850,000 kila mmoja. Zawadi nhii itakuwa ni kivutio kwa
wanariadha mashuhuri kushiriki katika mbio hizi zinazoingia mwaka wa 11 tangu
kuanzishwa.