Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akizungumza leo
KAMATI ya utendaji ya klabu
ya Simba imewafuta uanachama viongozi na tawi maarufu la Mpira Pesa, sambamba
na kuzivunja kamati zake ndogondogo.
Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage, amesema kamati ya
utendaji ya Simba iliyokutana juzi ilifikia maamuzi hayo baada ya kutokea kwa
chokochoko katika siku za hivi karibuni.
Alisema mwenyekiti wa tawi hilo , Masoud Awadh na
Katibu wake Ali Bane walikiuka katiba ya Simba kwa kuongea hovyo na vyombo vya
habari sambamba na kuitisha mkutano wa wanachama bila ya kupata ruhusa ya
uongozi.
Rage aliongeza kuwa Awadhi si
mwanachama hai wa klabu hiyo kutokana na kutolipa ada ya uanachama kwa zaidi ya
miaka miwili, huku barua yake aliyouandikia uongozi kwa niaba ya Simba nayo ni kinyume na katiba
kwani hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Tawi la Mpira Pesa chini ya
Awadhi lilifanya kikao cha kushinikiza Rage na viongozi wenzake kuachia ngazi
baada ya timu kufanya vibaya katika mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza wa
ligi kuu ya Vodacom na kuishia nafasi ya tatu.
Kama hiyo haitoshi, wanachama
wa tawi hilo
waliorodhesha majina zaidi ya 600 ili kutimiza akidi inayoruhusu kufanyika kwa
mkutano wa dharula wa Simba.
Hata hivyo, Rage alisema uongozi
umebaini kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wanachama waliojiorodhesha ni wafu, huku
pia saini zilizowekwa ni za kughushi.
Kuhusiana na kamati ndogondogo,
Rage alisema uongozi umeona hazina msaada wowote kwa timu hivyo hivi karibuni
ataunda kamati nyingine zitakazosaidia timu kupata ushindi.