SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF)
limezitaka timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za vilabu vya ligi kuu
bara, kujiandaa vema kwa ajili ya michuano ya ‘Uhai Cup’ inayotarajiwa kuanza
kutimua vumbi Desemba 12.
Katibu Mkuu wa TFF Angetile Osiah amesema leo kwamba michuano hiyo ni muhimu katika mustakabali mzima wa maendeleo ya
soka hivyo vilabu vinapaswa kufanya maandalizi ya uhakika.
Alisema bila vijana soka haliwezi kuendelea
hivyo vilabu shiriki havinabudi kufanya maandalizi ya uhakika ili kuweza kuleta
ushindani katika michuano hiyo.
“Ni matumaini yangu vilabu vimeandaa timu
na si kukusanya vikundi vya wachezaji na kuvileta kushiriki kwani tunahitaji
timu iliyofunzwa na si kukusanya wachezaji na mwisho wa siku hakuna mafanikio
yoyote,”alisema
Angetile aliongeza kuwa ratiba ya michuano
hiyo itajulikana rasmi kesho jumamosi ambapo kutafanyika droo maalum kwenye ofisi za
Shirikisho hilo.
Timu zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na
mabingwa watetezi Simba, Yanga, Azam, Coastal Union, Mgambo Shooting , Mtibwa
Sugar, Polisi Dodoma, Kagera Sugar, African Lyon, Ruvu Shooting, JKT Ruvu, Tanzania
Prisons, Oljoro JKT na Toto African.

إرسال تعليق