Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inayodhamini Timu ya Taifa (Taifa Stars) akisalimiana na Nahodha wa Taifa Stars Juma Kaseja wakati wa hafla fupi ya kuzungumza na wachezaji jana kabla ya mechi dhidi ya Ivory Coast. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Jakaya Kikwete amewataka wachezaji wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’
kucheza kwa nguvu zote kesho dhidi ya Ivory Coast na hatimaye kuibuka na
ushindi.
Stars na Ivory Coast zitakwaana keshokutwa kwenye uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa
kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia zitakazopigwa mwakani nchini Brazil .
Akizungumza kwa niaba ya
Rais, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mecky Sadick alisema kwamba, Kikwete
aliridhishwa na mchezo waliounyesha walipokwaana na Morocco wiki iliyopita licha ya
kufungwa mabao 2-1.
Alisema anaamini kikosi cha
Stars kipo tayari kwa mchezo huo baada ya kufanya maandalizi mazuri hivyo kazi
iliyobaki ni kutumia vema uwanja wa nyumbani hiyo kesho na kushinda.
“Rais amenituma kwenu nije
kuwaambia kwamba alifurahishwa na jinsi mlivyocheza dhidi ya Morocco wiki
iliyopita, pamoja na kufungwa kwenu amekisifu kikosi hiki hivyo amewataka
kutokata tamaa katika mchezo wenu wa Jumapili,”alisema Sadick
Awali, Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah amesema kwamba kikosi cha
Stars kilichopiga kambi kwenye Hoteli ya Tansoma kipo tayari kwa mchezo huo,
huku akiwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia.
Aidha, kiungo wa Stars Mrisho
Ngasa naye kesho ataukosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi mbili
za njano.