Waamuzi wote wa daraja la kwanza (Class I) wanaotaka
kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 wanatakiwa kuhudhuria
mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) utakaofanyika katika vituo
viwili.
Mtihani huo utafanyika Agosti 12,13 na14 mwaka huu katika
vituo vya Dar es Salaam
na Morogoro. Kituo cha Mwanza kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Geita,
Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Singida na
Tabora.
Kituo cha Dar es Salaam kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya
Arusha, Dar es Salaam , Dodoma ,
Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga.
Washiriki wote wanakumbushwa kuwa ni lazima wafuate
utaratibu huo wa vituo, na si vinginevyo. Pia waamuzi waliofungiwa (sio maisha)
wanatakiwa kushiriki katika mtihani huo.
RATIBA LIGI DARAJA LA KWANZA
AGOSTI 14
Ratiba ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2013/2014
inayoshirikisha timu 24 zilizo katika makundi matatu zikicheza kwa mikondo
miwili (nyumbani na ugenini) inatarajiwa kutolewa Agosti 14 mwaka huu.
Kundi A linaundwa na timu za Burkina Moro ya Morogoro, JKT
Mlale (Ruvuma), Kimondo SC (Mbeya), Kurugenzi Mufindi (Iringa), Majimaji
(Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Polisi (Iringa) na Polisi (Morogoro).
African Lyon (Dar es Salaam), Friends Rangers (Dar es
Salaam), Green Warriors (Dar es Salaam), Ndanda (Mtwara), Polisi (Dar es
Salaam), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp (Dar es Salaam) na Villa Squad
(Dar es Salaam) zinaunda kundi B.
Timu za kundi C ni JKT Kanembwa (Kigoma), Mwadui
(Shinyanga), Pamba (Mwanza), Polisi (Dodoma), Polisi (Mara), Polisi (Tabora),
Stand United (Shinyanga) na Toto Africans (Mwanza).
Tunapenda kukumbusha kuwa dirisha la usajili kwa madaraja
yote ni moja ambapo usajili wa hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 3
mwaka huu wakati hatua ya pili ni Agosti 14 hadi 29 mwaka huu. Dirisha dogo
litafunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.