Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili kufanya uamuzi wenye manufaa kwa washabiki wa mpira wa miguu baada ya tarehe ya uchaguzi aliyotangaza kuingilia na mechi ya watani wa jadi (Simba na Yanga) ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Sekretarieti ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira wa miguu wakiomba matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na Yanga) yafanyike katika siku tofauti.
Wakati Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu tayari ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha kuwa timu ambazo zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu zitacheza siku hiyo.
Sekretarieti imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa vile yeye na kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Uchaguzi. Huko nyuma TFF imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu ya Taifa (Taifa Stars), jambo ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo kuwa na ajenda moja tu.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha kikao cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.