Na Dina Ismail
NYOTA ya kiungo wa zamani wa Simba Mwinyi Kazimoto imezidi
kung’ara na huenda akashiriki ligi ya
mabingwa bara la Asia , imefahamika.
Hatua hiyo inafuatia nyota huyo kuwaniwa na mabingwa wa soka
wa Qatar, Al Saad ambao tayari wameshaanza mazungumzo na klabu ya Al Markhiya
ya huko kwa ajili ya kumnunua nyota huyo.
Hivyo basi, kama Kazimoto atasajiliwa na Al Saad atakuwa ni
mmoja ya wachezaji watakaopeperusha bendera ya Qatar katika ligi hiyo..
Habari kutoka Qatar zinaeleza kwamba, Kazimoto aliyejiunga
na Al Markhiya mwezi Agosti mwaka huu amekuwa gumzo nchini humo kutokana na
kiwango cha hali ya juu anachokionesha
pindi awapo dimbani.
Imeelezwa kwamba
mbali na mabingwa hao,Kazimoto pia anawaniwa na washindi wa pili wa Ligi
ya Qatar, Al Gharaf hivyo kazi itabaki kwa timu yenye dau kubwa kumchukua.
Habari hizo zimeongeza kwamba, tayari Kazimoto ameifungia mabao matatu timu yake
katika mechi saba ilizocheza wakati wa ziara maalum nchini Tunisia na Oman.
“Kwa kweli kiwango cha Kazimoto kimekuwa kikiiimarika siku
hadi siku kiasi ambacho viongozi wa timu kubwa wanaanza kumuwania,”alisema mtoa
habari huyo
Kazimoto amesajiliwa
Al Markhiya kwa miezi 18 kwa dau la dola
40,000.