GUMZO la wiki hii katika medani ya soka ni suala la uchaguzi wa viongozi wa klabu ya Yanga unaotarajiwa kufanyika Jumapili katika Ukumbi wa PTA uliopo ndani ya viwanja vya maonyesho ya Mwalimu Nyerere (zamani Sabasaba).
Wagombea katika uchaguzi huo wanaendelea na kampeni za kujinadi kwa wanachama wa klabu hiyo kwamba wataifanyia nini kama watachaguliwa Julai 18.
Kati ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, ni Francis Mponjoli Kifukwe atakayechuana na Mbaraka Hussein Igangula, Lloyd Nchunga, Edgar Chibula na Abeid Abeid ‘Falcon’.
Kwa upande wa Kifukwe, si jina geni masikioni mwa Wanayanga, kwani aliwahi kuiongoza klabu hiyo katika miaka ya nyuma akiwa rais wa klabu hiyo, hivyo kila mmoja anamfahamu vizuri kiasi cha kuwarahisishia kama ni kumpa kura au la.
Kwa upande wake, anasema amepanga kuivusha Yanga kutoka ilipo hadi kwenye mafanikio, akimaanisha kuifanya Yanga iwe na hadhi sawa na klabu nyingine kubwa Afrika kama Enyimba ya Nigeria, Al Ahly ya Misri, Supersport ya Afrika Kusini na nyinginezo.
“Nimeshaanza mikakati hiyo kwani nimerudi kwa kasi zaidi ili kujenga jeshi lenye sura mpya na nguvu zaidi, kwa pamoja na jeshi langu tunafanya jitihada za kuhakikisha wachezaji wetu wazuri wanaotaka kuondoka, hawaondoki,” anasema.
Kama hiyo haitoshi, Kifukwe anasema chini ya uongozi wake atahakikisha wachezaji pamoja na walimu wao wanakuwa na maisha bora, kwani anaamini kuwathamini watu hao ndio mtaji wa ushindi na mafanikio.
Agenda nyingine anayokuja nayo Kifukwe ni migogoro, anasema suala hilo limekuwa ni sehemu ya maisha ya Yanga tangu mwaka 1976 ulipoibuka mgogoro mkubwa ulioigawa klabu na kuzaa Pan African.
“Migogoro imeendelea kwa miongo yote miwili iliyofuata (miaka ya 1980 na miaka 1990), lakini tangu nimekuwa kiongozi Yanga, kwanza mjumbe wa Bodi ya Seneti, chini ya Rais Tarimba Abbas nilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunamaliza migogoro,” anasema.
“Kama mtakumbuka kulikuwa kuna vikao vya usuluhishi wa migogoro baina ya Yanga Kampuni na Yanga Asili ili kuirudisha Yanga moja, vikao hivyo viliihusisha hadi Ikulu, katika utawala wa Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa na baadaye wapenzi wengine wa klabu yetu kama Mzee Reginald Mengi pia walijaribu kutusaidia katika hili, lakini jitihada zao ziliishia njiani,” anaongeza.
Anasema akiwa Rais wa Yanga aliendelea na juhudi za kuhakikisha migogoro inamalizika na hatimaye walimpata Manji ambaye alifanya jitihada kubwa na wakafanikiwa kumaliza mgogoro huo na kujenga mwafaka.
“Kwa sasa naona kuna dalili za makundi kurejea ndani ya Yanga, hivyo nikifanikiwa kuwa mwenyekiti nitaanzia pale nilipoachia kwenye mwafaka. Nitaitisha mkutano wa wanachama tulijadili hili,” anasema.
Aidha, Kifukwe anasema Yanga kwa sasa haina dira, mambo hayaendi kama inavyotakikana kufanyika, hasa ukichukulia Yanga ni klabu kubwa Afrika, pia yapo mambo mbalimbali ambayo kama akiwa mwenyekiti atayafanyia kazi kwa maslahi ya Yanga.
Pia atahakikisha wanapitia upya Katiba na kuifanyia marekebisho, pia mradi wa soka ya vijana (Academy), kwa kukumbuka waliwahi kufanikiwa kutoa vipaji vya akina Mohamed Yahya ‘Tostao’, Juma Pondamali, Mohamed Adolph ‘Rishard’ na wengine katika awamu ya kwanza chini ya Profesa Victor na baadaye kina Anwar Awadh, Nonda Shabani, Maalim Saleh ‘Romario’, awamu ya pili chini ya marehemu Tambwe Leya.
Kifukwe pia amedhamiria kuifanya Yanga ijitegemee kwa kutumia rasilimali zake kama majengo, uwanja na nembo yake na wafadhili na wadhamini watabakia kuwa watu muhimu kwenye klabu, lakini lazima klabu iwe na misingi yake imara.
“Tayari nimekwishazungumza na wataalamu wa ubunifu wa miradi na masoko, kuhakikisha klabu inakuwa na vitega uchumi madhubuti, kuitumia nembo yetu, majengo yetu na uwanja kwa manufaa ya klabu. Si kama ilivyo sasa, vipo kama wakfu,” anasema.
Mbali ya hilo, Kifukwe anasema iwapo atachaguliwa kuwa mwenyekiti watapanua wigo wa taasisi yao kwa kuanzisha mfuko wa akiba na mikopo kwa wanachama (SACCOS), ambao utakuwa ukitoa mikopo kwa wanachama wake, kupitia matawi.
SOMA GAZETI TANZANIA DAIMA