MAZWILE
“NIKIWA kama ofisa mikopo wa Benki ya NMB, iwapo nitachaguliwa kuiongoza Yanga, kupitia fani yangu, nitaisaidia klabu yangu kujiinua kiuchumi kwa njia mbalimbali.”Hiyo ni kauli ya Isaac Mazwile, mmoja wa wagombea nafasi ya ujumbe katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga uliopangwa kufanyika Jumapili ijayo kwenye ukumbi wa PTA.
Katika mahojiano, Isaac anaanza kwa kusema Yanga ni yenye mtaji mkubwa wa rasilimali watu na mali, hivyo ikiwa na nguvu ya kiuchumi, wataanzisha Saccos itakayoweza kukopeshwa kati ya sh bilioni tatu hadi tano, hivyo kuleta manufaa kwa wote.
Anasema soka ya sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa na kwamba maendeleo halisi, hayatafikiwa bila klabu hiyo kuwa na nguvu kiuchumi, hivyo ni lazima ziwepo njia mbadala za kuiwezesha Yanga kujiendesha.
Mbali ya hilo, Isaac anasema iwapo atafanikiwa kutwaa nafasi hiyo, atahakikisha kunaanzishwa ‘Yanga Funs Social Club’ ambayo itatoa nafasi kwa wanachama wa klabu mikoani kukutana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Yanga.
“Hiyo itakuwa ikifanyika kikanda ambapo kila kanda kutakuwa na viongozi watakaosimamia hilo na mambo yatakayojadiwa watayawasilisha kwa viongozi,” anaongeza.
Aidha, atapigania Yanga kuanzisha maktaba itakayokuwa ikihifadhi kumbukumbu mbalimbali za klabu ikiwemo wachezaji ama mechi za Yanga, hiyo kuleta urahisi hata watakapotaka kuuza mchezaji nje ya nchi.
Isaac anaungana na wagombea wengine kuwa na nia ya kurekebisha katiba katika maeneo ikiwemo nafasi ya ujumbe ambapo katiba hiyo haianishi majukumu yake.
“Mfano ingekuwa wanachama wa Yanga (mikoa) ingegawanywa katika kanda hivyo kila mjumbe akapewa jukumu la kusimamia kanda moja, itakuwa ni rahisi sana katika utendaji,” anasema.
Kama hiyo haitoshi, Isaac anasema kupitia nafasi hiyo, kwa kushirikiana na viongozi watakuwa wakiwatafuta viongozi wa juu serikalini ili kuisaidia timu hiyo.
“Wenzetu Simba wamekuwa wakifanikiwa sana kwa njia hiyo kwani muda mwingi wamekuwa karibu na viongozi wa serikali, mashirika na makampuni binafsi na matokeo yake yanaonekana,” anaongeza.
“Pia nina haki ya kuwania nafasi hii baada ya kuisaidia Yanga kwa muda mrefu nimeona nijitose kuhakikisha naendeleza yale ambayo hayajafanywa na uongozi pamoja na kufanya mambo makubwa, nawaomba wanachama wa Yanga wanipe kura zao ili niwaletee mabadiliko,” anasisitiza.
Kabla ya kuwania nafasi hiyo, Isaac amekuwa karibu na klabu hiyo kwa namna moja ama nyingi, pia amewahi kuongoza kamati za michezo za timu mbalimbali hivyo ana uzoefu wa kuongozi.
Amewahi kuwa mratibu wa timu ya Wilaya ya Newala, katibu wa timu ya Mwenge Shooting ya jijini Dar es Salaam.
Anasema kutokana na kipaji chake katika michezo, alijikuta akisoma bure kuanzia sekondari mpaka chuo kikuu huku akiwahi kuzichezea timu za shule, Buibui FC ya Kinondoni, Maji ya Uganda na nyinginezo akichezea nafasi ya ulinzi.
Enzi zake aliwahi kucheza na baadhi ya nyota kama Lameck Sichula, Ali Saleh Omary, Anwar Awadh na wengineo.
Alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na kusoma Shule ya Msingi Bunge, kabla ya kwenda Uganda na kusoma Sekondari ya Budo na kidato cha tano na sita alisoma Kitande Hill pia ya Uganda.
Isaac ambaye kwa sasa ni Ofisa Mikopo wa Benki ya NMB Tawi la Kariakoo, alipata shahada ya kwanza ya Uongozi katika Chuo Kikuu cha Makerere, pia alisomea masuala ya biashara na teknolojia katika chuo cha IIT.
SOMA GAZETI TANZANIA DAIMA