HARUNA MOSHI 'BOBAN'
“Aprili mwaka huu, tulipokea taarifa kuwa Haruna anataka kuvunja mkataba na walipomuuliza kwanini, alisema hakuwa tayari kukatwa kodi na kwamba hakuwa akiridhishwa na mazingira ya timu ile, pia kutaka apatiwe sehemu ya mapato ya kiingilio kwa kila mechi,”amesema Damas Ndumbaro, Mkurugenzi wa Ndumbaro Soccer Agent (NSA) iliyompelea Boban Sweden.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Ndumbaro amesema mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania aliyekuwa akikipiga klabu ya Gefle If ya Sweden, ni mali na anayemtaka atalazimika kulipa dola 55,000 za Marekani na hiyo inafuatia Haruna Moshi 'Boban kuvunja mkataba wake wa miaka miwili kuichezea klabu hiyo.
Alisema klabu yoyote itakayotaka kumsajili inatakiwa ilipe kiasi hicho ambacho ni sawa na sh mil. 77 za Tanzania kwani NSA inashikilia haki za uhamisho ambazo ni dola 50,000 na dola 5,000 za masuala ya utawala.
Akifafanua sababu zilizofanya Boban kukatisha mkataba wake na klabu hiyo ya Sweden, alisema: na kuongeza Haruna alianza kutokwenda mazoezini akisingizia kuumwa na matokeo yake kocha akawa hampangi katika mechi, kwa mazingira hayo, kilichofuata kwa Boban ni kumweleza kocha wake hataki kuichezea timu hiyo.
“Kutokana na uwezo wa Boban, kocha alimwambia angemfanyia mpango katika timu nyingine, lakini Haruna alikataa na Julai 4, alisaini makubaliano ya kuvunja mkataba,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Ndumbaro alisema kitendo cha mchezaji huyo kuvunja mkataba kimemkosesha kuingia katika rekodi ya kuwa nyota wa kwanza Tanzania kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, pia kucheza na Livepool.
Kabla ya kujiunga na timu hiyo Boban alikuwa akiichezea klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.
Kwa sasa baadhi ya wadau wa Yanga wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu hiyo wapo katika mchakato wa kumsajili mchezaji huyo ili akipige Jangwani katika msimu mpya.