THIERY HENRY ATIMKA RASMI BARCA, AJIUNGA NA NY RED BULLS YA MAREKANI


THIERY HENRY

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Thierry Henry, aliyekuwa akichezea timu ya FC Barcelona ya Hispania, ameihama na kujiunga na timu ya New York Red Bulls ya Ligi Kuu ya Marekani, Major Soccer League ‘MSL’.


Henry (32), aliyeichezea Ufaransa mechi 123 na kuifungia mabao 51, alijiunga na Barcelona mwaka 2007 akitokea Arsenal ya England aliyojiunga nayo mwaka 1999.

Akiwa Arsenal, Henry aliweka rekodi ya kuwa nyota wa kwanza wa Ufaransa kupata mafanikio makubwa katika klabu ya Arsenal akiifungia mabao 226 katika mechi 370 na kuiwezesha kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu na matatu ya Kombe la FA.


THIERY HENRY

Mbali ya mafanikio hayo, Henry ni kati ya nyota waliokuwamo katika kikosi cha Ufaransa kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1998 na Kombe la Mataifa Ulaya miaka miwili baadaye.

Hata hivyo, Juni 2007, Henry aliondoka Emirates na kutua Nou Camp kwa kitita cha pauni mil. 16.1 na kuifungia timu hiyo mabao 49 ndani ya misimu mitatu.

Katika kipindi hicho, Barcelona imetwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ‘La Liga,’ ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa Super Cup na Klabu bingwa ya Fifa.

Julai 22, Henry anatarajiwa kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza katika mechi ya kirafiki dhidi ya Tottenham ya England mechi itakayochezwa Marekani.

Akizungumzia kuondoka kwake, Henry amesema ni furaha kubwa kufungua ukurasa mpya katika maisha ya soka. Henry ni kama anafuata nyota za David Beckham, nyota wa kimataifa wa England ambaye alihamia Real Madrid ya Hispania akitokea Manchester United kabla ya kutimkia klabu ya Los Angeles Galaxy ya Marekani.

Post a Comment

Previous Post Next Post