MWENYEKITI WA YANGA LLOYD NCHUNGA AKIKABIDHI MIFUKO YA SARIJI KWA WANACHAMA WA TAWI LA YANGA KURASINI
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mifuko hiyo kwa ajili ya ukarabati wa tawi hilo, Nchunga alisema anafanya hivyo kwa lengo la kuimarisha matawi kama alivyoahidi.
Alisema kama matawi yatakuwa imara itakuwa ni njia rahisi ya kujenga umoja ambao utasaidia kuwepo kwa maendeleo katika klabu hiyo.
Nchunga alisema tawi hilo ni mwanzo tu kwani anakusudia kutoa mchango katika matawi mengine ya jijini Dar es Salaam huku leo mchakato huo ukiendelea kwa matawi kadhaa.
“Tunataka kuyasapoti matawi ili wanachama pia waongezeke, nimetoa mchango huu kama mwanzo wa kuanza kutekeleza ahadi zangu wakati nilipokuwa natangaza sera zangu na kuomba kura,” alisema.
Aidha, Nchunga aliwashukuru wanachama wa tawi hilo na wengine wote ambao walimpigia kura zilizomuwezesha kushika wadhifa huo.
Msaada huo ulipokewa na Makamu Mwenyekiti wa tawi hilo, Mustafa ambaye pamoja na kumshukuru, aliahidi kushirikiana naye katika kuhakikisha Yanga inakuwa kitu kimoja, sambamba na kupata mafanikio.
Naye mmoja wa wanachama wa Yanga, Athuman Rashid, alimsihi Nchunga kuteua katika kamati yake viongozi wanaofanya kazi kwa utaratibu mzuri, wenye malengo mema na klabu na si wababaishaji.
“Tunakuomba uteue viongozi wenye uchungu na mafanikio ya Yanga, tumechoka kufungwa, tunataka na sisi klabu yetu iwe na mafanikio,” alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na mwenyekiti wa kamati ya kuratibu matawi Tito Osoro pamoja na mjumbe wa kamati hiyo na Kamati ya Utendaji, Sarah Ramadhan.