SHILOLE:NYOTA WA BONGO MUVIE ANAYECHUKIZWA NA WAVUA NGUO ILI WAUZE SURA





KUKUA kwa tasnia ya filamu Tanzania kunakwenda sambamba na kuibuka kwa vipaji vipya vya waigizaji mahiri na wenye mvuto kila kukikcha.


Mmoja kati ya Zena Mohamed Yussuf maarufu kama ‘Shilole’ ambaye tangu ajikite katika tasnia hiyo ameweza kuonyesha uwezo na kiwango cha hali ya juu licha ya kuwa amecheza filamu nne ambazo zimeshatoka mpaka sasa .

Kwa wanaofuatilia filamu hizo watakumbuka jinsi alivyofanya kweli katika ‘Fair Desecion’ akicheza na Ray, Johari na wengineo,ikifuatiwa ‘Crazy Of Love’ aliyocheza na Basupa, David Mjata na wengineo, ‘Pigo’ aliyocheza na Cloud na Aunty Ezekieli kabla ya kuibukia katika ‘Bed Rest’ akicheza na Ray, Thea, Johari na Mainda.

Hivi karibuni msani huyo ataonekana katika filamu mpya iliyosheheni nyota kibao katika nyanja mbalimbali nchini ‘Cut Off’ ambayo ipo katika matayarisho ya mwisho mwisho kabla ya kuingia sokoni.

Filamu hiyo kali na ya kusisimua mbali na Shilole pia imeigizwa na wakali wengine wakiwemo Rose Ndauka, Cloud, Cheki Budi, Aunty, Darleen na wengine.

Akizungumzia tasnia nzima ya sanaa ya filamu nchini anasema kwamba imeonekana kuvamiwa kutokana na baadhi ya watu kuamua kujikita baada ya kuoana wamekosa kazi ya kufanya,huku pia wakiwa hawana vipaji hali ambayo inafanya sanaa hiyo idharaurike na kuonekana ya wababaishaji.

“Kiukweli sanaa yetu inapanda lakini kuibuka kwa watu kibao kila mmoja akijifanya msanii wakati hana kipaji kunatutilia doa na kufanya tuonekane waigizaji wote ni wababaishaji”, Anasema.

Shilole, likiwa na maana ya kioo alilopewa na bibi yake anasema kabla ya kufikia hapo alipo alipitia milima na mabonde katika kazi yake kitu anachokiona kuwa ni changamoto katika maisha yake ambavyo pia anaamini vinasaidia katika kuboresha na kukuza kipaji alichonacho.

Pamoja na hilo anasema hakukata tamaa kwani amedhamiria kuhakikisha anakuwa msanii mwenye jina kubwa zaidi alilonalo nje ya Tanzania na mipango yake zaidi kucheza hadi Hollywood.

“Ninataka kuwa first lady wa bongo movie siku moja, hilo linawezekana kwani ni moja ya dhamira yangu katika medani hii”, Anasema Shilole ambaye kabla ya kufikia hapo aliwahi kupitia katika kikundi kilichokuwa chini ya mpiga gitaa wa kundi la Jahazi Modern Taarab, Thabit Abdul ‘Mtoto wa Ilala’.

Akizungumzia hali ya sanaa hiyo kwa sasa anasema imekuwa ikikuwa kwa kasi kwa pamoja na kuibuka kwa waigizaji wengi, hata kipato wanacholipwa kimepanda akitolea mfano yeye alianza kucheza kwa ujira mdogo wa sh.20,000 lakini kwa sasa analipwa mpaka sh. 300,000 na kuendelea kwa ajili ya kazi hiyo.

Anaongeza kuwa kuibuka huko kwa wasanii kumeleta ushindani huku akimtaja Aunty Ezekiel kama ni mwanadada mkali zaidi katika movie za kibongo, huku kwa upande wa kiume akimtaja Vincent Kigosi ‘Ray’.

Msanii huyo anatoa ushauri wa bure kwa kuwataka wasanii waliokimbilia kuigiza kwa mapenzi yao tu bila ya kuwa na vipaji kuacha mara moja na kufanya vitu walivyo na vipaji nanvyo akimtolea mfano msanii wa bongo Fleva, Hemed Suleiman na kusema kwenye bongo fleva ndio nyumbani kwake.

Wasanii wengi wa kike wamekuwa wakidaiwa kutowakataa ‘mapedeshee’ pindi wanapowatokea analizungumziaje?

“Ni kweli wasanii wengi wa kike hawajui kukataa wanaume na hasa wenye fedha, ila si wote na mimi si miongoni mwao, kwani wanaokubali hali hiyo wengi ni malimbukerni ambao wamekuja mjini hawaijui fedha, wakihongwa laki laki mbili wanachanganyikiwa”, Anasema.

Anasema vishawishi ni vingi sana kwao kutokana na kazi wanayoifanya hivyo hawana budi kujiuliza kwanza badala ya kukurupuka kijinga kwenye masuala ya mapenzi vinginevyo itakuwa mwisho mbaya.

“Yaani hapo tunatakiwa tuwe na umakini wa hali ya juu wengi wanataka kututumia tu kwa starehe za muda mfupi na wakishakidhi haja zao wanakuacha, mimi alinijia mtu kwa ahadi lukuki, yaani kunijengea nyumba ndani ya siku mbili na kadhalika, kwa kweli nilishtuka na kumtimua na fedha zake”, Anasema.

Akizungumzia suala la ngono ambalo limekuwa likitawala katika medani hiyo, msanii huyo anasema kwa upande wa wasanii kwa wasanii mengi yanatokea nyuma ya jukwaa, lakini dawa ya hilo ni kuepukana na hali ya kuweka ukweli katika kuigiza na kusema kwamba yupo tayari kurejesha fedha alizopewa kwa ajili ya kuigiza sehemu kama hizo kuliko kujitafutia balaa.

Kwa upande wa watayarishaji na rushwa ya ngono, Shilole anasema wapo baadhi wenye tabia hiyo kwani hata yeye iliwahi kumtokea lakini alikataa na mwisho wa siku kazi ilifanyika na mpaka amefikia hapo alipo hajatoa penzi ili apewe nafasi ya kucheza filamu.

“Wasanii na hasa wa kike tujiamini, tusikubali kuvuliwa nguo kwa ajili ya kutaka kutoka, sawa utatoka katika filamu ya kwanza, je ya pili na ya tatu je utatoka kwa kuvua nguo? Tuwe imara kwa kujiheshimu kwa kufanya hiyo dhalili itatoweka”, Anasema.

Msanii huyo mwenye mtoto mmoja aitwaye Rahma mwenye umri wa miaka mitano aliyemzaa na mumwe Twaha Rahamadhan aliyefunga naye ndoa mwaka 2005 kabla ya kutalikiana miaka mitatu baadaye, alizaliwa huko Igunga, Tabora mwaka 1986.

Elimu yake ya msingi na Sekondari aliipata Igunga kabla ya kuja Jijini Dar es Salaan na kujiunga na Chuo kimoja cha masuala ya hoteli na utalii kilichopo Magomeni alipopata cheti ambapo mbali na filamu anafanya kazi ya uhudumu katika hoteli ya Peakock iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Akiwa anavutiwa na muigizaji wa Kinigeria Ini Edo, Zena ni mtoto wa mwisho kati ya familia ya watoto watano, huku wazazi wake Mohamed Yussuf na mama Pili Yussuf walifariki wa ajali ya gari ya abiria, walipokuwa wakisafiri kutoka Igunga kwenda Tabora mwaka 1996.



WASIFU WAKE:

JINA: Zena Mohamed Yussuf

KUZALIWA: Agosti 19, 1986

ALIPOZALIWA: Igunga, Tabora

SANAA: Uigizaji

ANAPOISHI: Mabibo

1 Comments

  1. Hongera zake na huu ni mwanzo mzuri kwani kama wasanii wenyewe wameshaligundua hilo , basi sio tatizo kubwa, ni swala la kuangalia nani anafaa na nani hafai, wisho wa siku mnakuwa na watu wazuri kwenye kikundi auu vipi

    ReplyDelete
Previous Post Next Post