MMOJA YA WAUGUZI WA WODI YA WANAUME, MOHAMMED SULEIMAN
MADAKTARI WA KUJITOLEA KUTOKA NCHINI CUBA
WODI YA WANAUME
NI mara chache sana kusikia mtu, kikundi cha watu ama shirika limetoa msaada katika hospitali ya watu wenye matatizo ya akili na hasa ikizingatiwa kuwa watu wanaotibiwa huko wanahitaji kupata huduma zinazostahili, ukaribu na ufuatiliaji wa hali ya juu.
Lakini hiyo ni tofauti na hospitali ya watu wenye matatizo ya akili iliyopo Visiwani Zanzibar ambayo licha ya kuwa na umuhimu wake kwa jamii lakini jamii inayoizunguka imeshindwa kuijali na kuithamini hivyo kuifanya isiwe na taswira kama ni hospitali ya watu maalum.
Kutokana na hali halisi Maryan Olsen kwa miaka mitatu sasa amekuwa akiisaidia hospitali hiyo kwa namna moja ama nyingine ili mradi kuhakikisha hali ya mazingira ya ndani na nje vinakuwa bora, ili kuwafanya wagonjwa wasijiskie faraja pindi wanapokuwa hospitalini.
Kupitia kampuni yake ya Explore Zanzibar tangu mwaka 2008 amekuwa akiaandaa onyesho la hisani la kuchangia fedha kwa ajiri ya kuboresha hospitali hiyo ambapo kwa asilimia 70 ameweza kubadilisha mazingira ya hospitali hiyo kutoka katika uchakavu mpaka kuwa na taswira ya kuvutia.
Akizungumza visiwani humo mwishoni mwa wiki iliyopita Maryan alisema kwamba akiwa kama Mzanzibar analojukumu na wajibu wa kuwapatia maisha bora watu wa hali hiyo ambao wanaonekana kama wametengwa katika jamii inayowazunguka
Alisema mara nyingi jamii imekuwa ikiwasahau watu wa namna hiyo na kuwapa kipaumbele makundi mengine ya watu hivyo ameona ni muhimu kuendeleza mpango wake wa kuwasaidia akiwa anaamini kwamba siku moja malengo yatatimia kwani watu wa namna hiyo hawakuomba iwe hivyo.
Aliongeza kuwa fedha zilizopatikana katika onyesho la ‘Fashion For Health Black & Gold Gala Nite’ zitasaidia kukarabati wodi ya wanaume na kujenga kituo cha michezo kwani ni miaka mingi sasa wagonjwa wamekuwa wakikaa tu wodini bila ya kichocheo/ kiburudisho, hivyo kwa taratibu hali itabadilika.
Awali waandishi wa habari tulipata fursa ya kutembelea katika hospitali hiyo na kujionea mambo mbalimbali ikiwemo kuzungumza na baadhi ya watu wanaowasaidia wagonjwa ambapo kwa kiasi kikubwa walikuwa wakilalamika kutupwa mkono na serikali ambayo ina mamlaka ya kuisimamia hospitali hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema, hakuna viongozi yeyote wa serikali ambaye amekuwa akijitokeza walau hata mara moja kwa mwezi kwa ajili ya kwenda hata kuwajulia hali wagonjwa na pia kujua matatizo yaliyopo zaidi ya baadhi ya wasamaria wema kufika mara moja moja na kutoa misaada midogo midogo.
“Yaani kwa kweli inasikitisha sana hii hospitali utadhani siyo ya Serikali jamani, mazingira waliyopo si ya kuridhisha kabisa afadhali hata kidogo nasikia huyu dada amekuwa akijitolea kwa hali na mali chochote alichonacho na kuwapa wagonjwa au kukarabati baadhi ya maeneo, lakini hali si nzuri kwa kweli”, Alisema mmoja ya watu ambaye alikwenda kuwaona ndugu zake.
Kusema kweli hali tuliyoikuta hospitalini humo na hasa wodi ya wanaume si ya kuridhisha hata kidogo, uchafu, magodoro yaliyoharibika na hata wagonjwa wenyewe hali zao zilikuwa si za kuridhisha, ulinzi duni na wafanyakazi wachache tofauti na hali halisi ya huduma inayohitajika kwa wagonjwa.
Cha kusikitisha zaidi kuna wagonjwa wengine wametelekezwa na ndugu zao, ambapo mgonjwa mdogo zaidi akifahamika kwa jina la Cholo mwenye miaka 15 ambaye anadaiwa kudumu hospitalini hapo kwa zaidi ya miaka saba akiwa ametelekezwa na mama yake mzazi, lakini mwenyewe ameshazoea mazingira hayo anajiona kama yupo nyumbani.
Wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo wengi wao na hasa wavulana matatizo yao yanatokana na utumiaji wa madawa ya kulevya, pia ugonjwa wa malaria na matatizo ya kibinadamu ya kawaida vinatokea jinsia na rika zote, huku madaktari wachache waliopo wakisaidiwa na madaktari wa kujitolea kutoka nchini Cuba.
Pia wagonjwa hao wamegawanywa katika makundi mawili, wagonjwa ambao wana hali mbaya sana kiasi cha kuweza kudhuru wenzao, wao hutengewa sehemu yao na wagonjwa wenye nafuu nao hukaa sehemu tofauti.
Muuguzi wa zamu tuliyemkuta katika wodi ya wanaume, Mohammed Suleiman akizungumzia matatizo yaliyopo hospitalini hapo anasema moja wapo ni madawa ambapo kuna baadhi ya dawa kama Hloperido ambazo zimekuwa adimu kupatikana hivyo kufanya wagonjwa kushindwa kupata dozi ya uhakika, pia ukosefu wa vifaa.
Pia wagonjwa kukosa mlo kamili kwani hupata mlo wa asubuhi na mchana tu, hali ambayo si nzuri kwani dawa wanazopatiwa ni kali hivyo zinahitaji kupata mlo uliotimilika, lakini kuna baadhi ya wagonjwa huwa wanaletewa chakula na ndugu zao ambao huja kuwaona kwa nyakati tofauti, wasio na ndugu ndio wanaishi kwa ratiba ya milo miwili.
Tatizo jingine ni uangalizi wa familia ‘family support’ “mgonjwa baada ya kupata nafuu na kurudishwa nyumbani kuna dawa anapewa na nyingine hutakiwa kuijia baada ya muda fulani inabidi afuate dawa nyingine, lakini wakifika huko hakuna usimamizi na matokeo yake baada ya muda mchache mgonjwa anazidiwa na kurudishwa tena”, Anasema.
“Kuna baadhi ya wagonjwa wanatakiwa kunywa dawa katika maisha yao yote, kinyume na hapo ugonjwa unarejea tena sasas kama familia inashindwa kumsimamia mgonjwa ipasavyo matokeo yake ugonjwa unakuja kwa kasi na kufanya arejeshwe hospitali”, Anaongeza.
Akielezea changamoto anazokumbana nazo pindi anapokuwa kazini anasema ni nyingi sana hasa ikizingitiwa kuwa wagonjwa wa akili ni watu wanaohitaji uangalizi wa hali ya juu, kukaa nao kwa upendo na kutumia busara katika kuwapa maelekezo vinginevyo unawezakuta hali ya hewa inachafuka.
“Hawa watu ni watu wanaohitaji mtu mwenye moyo wa huruma na ukarimu vinginevyo kazi inaweza kukushinda, unatakiwa umuangalie mgonjwa vizuri na kumueleza mambo ambayo hayawezi kumpandisha hasira, si unajua tena mtu akipandwa na hasira anakuwaje, halafu pia anaugonjwa wa akili”, Anasema.
Aidha, muuguzi huo anasisitiza kwamba wagonjwa hao pia wanahitaji viburudisho kama redio, televisheni na hata sehemu za kuchezea kwani baadhi ya wagonjwa ambao akili zinaanza kuwarejea huwa wanauliza vitu kama hivyo.
Kwa upande wa wodi ya kinamama ambayo hali yake kiasi inaridhisha, mmmoja ya wake Riziki Salum Omary anasema licha ya kuwepo kwa wauguzi 32, lakini idadi hiyo haitoshelezi kwani kuna kipindi wagonjwa wafika hata 40 hivyo inakuwa hekaheka katika kuwahudumia.
Pia uhaba wa wodi, yaani kutokana na kuwepo kwa wodi moja inawawia vigumu kuwatenganisha wagonjwa wenye hali mbaya na wale wenye nafuu kitua ambacho si kizuri katika usalama wao.
Kwa ujumla pamoja na kupatiwa matibabu wagonjwa hao hupata fursa ya kufanya kazi za mikoni kama uchoraji, ufumaji na hata utunzaji wa bustani na wakati mwingine hujiburudisha kwa kucheza karata au bao.
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kupitia mfuko wa Vodacom Foundation, PSI, Africa Life Assurance, Explore Zanzibar, 361 Degrees Events, Vayle Springs Ltd na Mustafa Hassanali Courte zilidhamini onyesho maalum la kuchangia hospitali hiyo lilofanyika kwenye hoteli ya Serena Inn huku likipambwa na bendi ya muziki ya Tanzanite.
Inasikitisha sana, wagonjwa wote wanatakiwa wajaliwe, awe na upungufu wa akili awe na matatizo mengine wote ni wagonjwa, hatutakiwi kuwabagua. Hawa wenye matatizo ya akili wengine wanafukuza kabisa na kuwa ombaomba mitaani.
ReplyDelete