NEY WA MITEGO
KUTOA ni moyo, wala si utajiri, walisema wahenga. Naam, usemi huo unadhihirishwa na msanii chipukizi anayeinukia kwa kasi katika muziki wa Bongo Fleva, akipiga mtindo wa Hip hop, Emmanuel Elibariki Munisi maarufu kama Ney wa Mitego ambaye ameamua mauzo yote yatakayotokana na albamu yake ya kwanza, yaende kuwasaidia watoto yatima wa kituo cha CMC kilichopo Chimala mjini Mbeya.Ney hakuhitaji kwanza kuuza muziki wake na kujilimbikizia fedha ndipo awasaidie wenye hali ngumu, bali ameamua moja kwa moja pato lake la kwanza liende kuwasaidia viumbe wa Mungu kama yeye waishio katika mazingira magumu.
Hapana shaka kijana amezingatia maandiko, kwamba ni rahisi ngamia kupenya kwenye tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia peponi, hivyo ameamua kwanza kuusaka ufalme wa mbinguni.
Katika mahojiano maalum, Ney anasema kwamba amefikia uamuzi huo baada ya kuguswa na matatizo waliyonayo watoto wanaolelewa kituoni hapo na tayari wamekwishachukua awamu ya kwanza ya mauzo ya albamu hiyo, ambayo ni sh milioni 2.5.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni ‘Itafahamika’, ‘Mitego’, ‘Kama Unanipenda’, ‘Nakutaka’ aliomshirikisha Mwasiti, ‘Nini Umependa’ aliomshirikisha Vumi, ‘Muziki’, ‘Jinsi’ na ‘Ningojee’ aliomshirikisha Matonya.
Umaarufu wa Ney unatokana na wimbo ‘Itafahamika’, ambao ndani yake amewapa vijembe wasanii waliokuwa juu kipindi cha nyuma, lakini kwa sasa wameporomoka kwenye chati, hususan wale ambao hata kiuchumi wametikisika vibaya.
“Sister P anauza pipi, Rah P muhudumu wa gesti, Dudu Baya kawa Mmanga, Mr. Nice anauza shanga,” hiyo ni baadhi ya mistari ambayo Ney anawananga wakali waliovuma miaka ya nyuma.
Ney wa Mitego anasema kwamba aliamua kuimba wimbo huo kutokana na kuufananisha muziki wa Bongo Fleva na mwanamke ambaye hajatulia, ndiyo maana kuna sehemu anasema; “Bongo Fleva kicheche, bongo fleva mapepe.”
Anasema wazo la kutunga wimbo huo lilikuja siku moja alipokuwa akisikiliza nyimbo za wasanii wa Bongo Fleva, zilizotamba miaka ya nyuma, ambazo kwa sasa walioimba hawatambi tena katika fani hiyo, hivyo mmoja wa marafiki zake alimshauri kutunga wimbo unaozungumzia hali hiyo.
Ney anasema kabla hajautoa, aliongea na Dudubaya na kumuelewesha kuhusu wimbo huo, lakini cha kushangaza baada ya kutoka msanii mwenzake huyo alimgeuka na kuanzisha vita dhidi yake kama ilivyokuwa kwa Inspekta Haroun, ambaye naye ametupiwa kijembe kwenye wimbo huo.
“Pia Afande Sele sikumtaja, lakini aliamua kununua ugomvi usiomhusu, lakini P Funk ambaye pia alitajwa katika wimbo huo hakuwa na la kusema zaidi ya kusema Ney ni mdogo kwangu hivyo sioni tatizo lolote akiniimba,” anasema Ney.
Wasanii wengine ambao aliwataja kwenye wimbo huo walimwelewa na kwa kuonyesha hawakuwa na kinyongo naye, aliwaita kwa ajili ya kuwashirikisha katika remix ya wimbo huo na walikubali - nao ni Sister P, O- Ten na Bwana Misosi.
Kwa kifupi wimbo huo ambao ulirekodiwa katika studio za Jaraman… ulimpandisha chati msanii huyo ambapo pamoja na kushika nafasi za juu katika chati za muziki za redio mbalimbali, pia ulimpatia mialiko ya shoo katika miji tofauti na hivyo kuona muziki ndiyo kazi.
Kabla ya wimbo ‘Itafahamika’ haujapotea masikioni mwa wadau wa muziki, Ney katikati ya mwaka huu aliachia kibao kingine kiitwacho ‘True Boy’, ambacho nacho kilikuwa gumzo kubwa kwenye tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, kutokana na ujumbe uliomo ndani yake, kwa mfano kuna sehemu anamzungumzia mchungaji mama Getrude Rwakatare juu ya kuchanganya kwake dini na siasa.
“Wavuta sigara sio wazima, hawana akili timamu kwani wanafahamu sigara ina madhara lakini bado wanaendelea kuvuta, vijana kutaka kwenda Ulaya wakati hawajui hata Kiingereza.” Hiyo ni sehemu nyingine ya mistari mitamu yenye kusisimua iliyopo kwenye wimbo huo.
Mwezi uliopita aliachia wimbo mwingine uitwao ‘Nini Umependa’, akimshirikisha Vumi, ambao ndani ndio uliisindikiza albamu yake ya kwanza sokoni, iitwayo ‘Ney wa Mitego.
Anasema kwamba, tayari amekwishaanza maandalizi ya albamu yake ya pili na muda si mrefu ataanza kutoa nyimbo za kuitambulisha. Katika albamu hiyo, anasema kwamba atawashirikisha wasanii wenzake kama Matonya, JP na Linah.
Akizungumzia hali ya muziki wa Bongo Fleva hivi sasa, Ney anasema kwamba bado umelala na wasanii wanahitaji kubadilika sana ili kuweza kupiga hatua, kinyume na hapo muziki wa kizazi kipya utazidi kuzorota na hatimaye kupotea kabisa.
“Unajua siku hizi wasanii wengi wanababaisha sana kazi zao kuanzia kutunga, kuimba hadi ala, kitu ambacho hakiwezi kuleta maendeleo, watu wanazungumzia mapenzi tu wakati jamii ina mambo mengi ya kuzungumzia, wasanii tubadilike.
“Mimi nimedhamiria kufika mbali katika medani ya muziki ndiyo maana hata nyimbo zangu naimba masuala mbalimbali yenye maana, ambayo kila mtu akiusikia anakubali ninalonena, pia nina uwezo wa kufanya aina yoyote ya muziki hivyo kazi hii haiwezi kunipiga chenga daima,” anasema.
Kwa mantiki hiyo Ney amewashauri wanamuziki nchini kuwa wabunifu, vinginevyo muziki wao utaishia hapa hapa, pia kuwa na umoja na mshikamano ambao anaamini ndiyo silaha ya mafanikio katika jambo lolote.
ALIKOTOKEA:
Ney alizaliwa Juni 9, 1986 Manzese, Dar es Salaam na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Ukombozi mwaka 1993 hadi 2000, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Mbezi Beach aliposoma kidato cha Kwanza hadi cha Nne mwaka 2001 hadi 2003.
Alianza kuupenda muziki tangu akiwa mdogo kabla ya mwaka 1993 kujitosa kwenye ‘game’ akianza kwa kuigiza nyimbo za wasanii nyota duniani kama Tupac Shakur (sasa marehemu), na nyingine za wasanii wa nyumbani kama Mr II Sugu na kundi la GWM lililokuwa likiundwa na wakali kama KR na D Chief.
Mwaka 1998 alirekodi wimbo wake wa kwanza uliokwenda kwa jina la ‘Hands Up’ katika studio za Marimba, lakini wimbo huo haukupata nafasi katika vituo vya redio nchini kwa sababu kipindi hicho muziki wa Bongo Fleva ulikuwa haupewi nafasi.
“Pamoja na kufanya muziki, nilikuwa kama naiba kwani nilikuwa bado mdogo nikisoma shule ya msingi, hivyo wazazi wangu hasa mama hawakupenda nijihusishe na masuala ya muziki, wakihofu nitashindwa kufanya vyema darasani,” anasema.
Anasema mwaka 1999 makundi ya Big Dog Pose (BDP) na HBC yalianza kusikika, hivyo naye aliamua kuanzisha kundi lililojulikana kama WAGADU akiwa na Nigga P, Kim J na Major, ambao kwa pamoja walirekodi wimbo mmoja katika studio za Sound Crafters, Temeke, Dar es Salaam.
“Nilikuwa natoroka nyumbani na kwenda kuhudhuria maonyesho ya wasanii wa Bongo Fleva katika Ukumbi wa Ruaha Galax, Kimara na huko nilikuwa nikiwaona kina Juma Nature, kundi la Gangwe Mob, Manzese Crew na wengineo ambao walitupa hamasa zaidi,” anasema.
Kutokana na msukumo huo, mwaka 2002 alitoa wimbo ambao kidogo ulivuma, ‘Ingekuwa Poa’, akimjibu Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ na wimbo wake ‘Ingekuwa Vipi’.
Wimbo huo ulimfanya apokewe na Patter Mathysse ‘P Funk’ wa studio maarufu za Bongo Records, zilizopo Mwenge, Dar es Salaam na akiwa huko, wimbo wake wa kwanza kutoa ulikuwa ni ‘Kama Unanipenda’. Lakini kitendo cha kurekodi wimbo huo, kilimchongea, kwani mama yake alipousikia alikasirika mno na kumfukuza nyumbani.
“Tangu nimetoka nyumbani nikiwa kidato cha pili nilikuwa nakaa tu ghetto na washkaji mpaka nikamaliza kidato cha nne na kuamua kujikita zaidi katika muziki, huku pia nikifanya biashara zangu nyingine, namshukuru Mungu ninapata vijisenti vya kuniweka mjini,” anasema.
Ney anasema mwaka 2005 alitoka na wimbo ‘Mitego’, ambao ulimtambulisha zaidi kwa Watanzania, kabla ya mwaka 2007 kuachia ‘Anza Kukatika’, ambao nao ulipokewa vizuri, na baada ya kimya kirefu mwaka 2009 akato ‘Itafahamika’.
Naam, huyo ndiye Ney wa Mitego, msanii aliyeamua kujitolea fedha zake zote za mauzo ya albamu yake ya kwanza kwa ajili ya watoto yatima. Je, wangapi kati ya waliotengeneza mamilioni kupitia muziki wana moyo kama huo? Kwa nini Mungu asimbariki na kumfungulia zaidi njia za mafanikio msanii kama huyu mwenye huruma na kuthamini?
WASIFU WAKE: