MABAO matatu yaliyofumgwa na mshambuliaji wake Mbwana Samatta, jana yaliiwezesha Simba kuvuna pointi tatu kutoka kwa Mtibwa Sugar kwa kuitandika mabao 4-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo sio umeiwezesha Simba kupata pointi tatu tu, pia kurejea katika kiti cha uongozi wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 21, mwaka jana ikishindanisha timu 12.
Simba iliyoshuka dimbani jana ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 34, sasa imekwea hadi nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 37, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 35 na Yanga pia yenye pointi kama hizo.
Hata hivyo, Simba wanaweza kupigwa kumbo katika nafasi hiyo kama mtani wake Yanga atashinda mechi yake ya leo dhidi ya Ruvu Shooting itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
Kama Yanga itashinda, itakamata usukani wa ligi hiyo kwani itakuwa na pointi 38, lakini kinyume cha hapo, itakuwa imetoa nafasi ya kupitwa na timu nyingine zinazoshindania nafasi tatu za juu.