NCHIMBI AKERWA NA USHIRIKINA KATIKA SOKA


SERIKALI imewataka waamuzi wa soka kuepuka kuwa sehemu ya kuvuruga soka ya Tanzania, badala yake wawe katika kuuendeleza mchezo huo.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwenye ukumbi wa NSSF Water Front jijini Dar es Salaam , Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi alisema waamuzi ndio nguzo ya maendeleo ya michezo, hivyo wanatakiwa kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha, Waziri Nchimbi alipiga vita matumizi ya imani za kishirikina ‘ndumba’ zilizokithiri viwanjani, kwa sababu zinaharibu maendeleo ya soka.
Alisema wachezaji na timu za Tanzania, waige mifano ya wenzao wa kimataifa kama kina Lionel Messi na Didier Drogba.
Waziri huyo alitoa mfano katika mashindano yaliyoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) hivi karibuni, ambapo kuna mdau mmoja alimfuata kumshauri masuala ya ndumba katika fainali hizo zilizochezwa jijini Dar es Salaam.
“Kuna jamaa alinifuata, walitaka kumuingiza mchawi uwanjani kumalizia kazi, lakini Kocha Mkuu, Jan Poulsen, alikataa na mimi pia nilikataa, jamaa baadaye alinipigia simu kuendelea kunibembeleza,” alisema Nchimbi.
Aliongeza kuwa bila kukataa ushirikina katika soka ya hapa nchini, matokeo yake ni kupoteza mwelekeo wa mchezo huo badala ya kupiga hatua.
Katika hatua nyingine, waziri huyo alitoa wito kwa wadhamini, kuendelea kuijali soka ya Tanzania, kwa kusaidia misaada mbalimbali na kutoa wito kwa mashirika mengine kujitokeza zaidi ili kufanikisha maendeleo.

Post a Comment

Previous Post Next Post