TIMU ZA LIGI KUU ZAVUNA MAMILIONI


BONIFACE WAMBURA, MSEMAJI TFF
MALIPO YA HAKI ZA TELEVISHENI
Klabu 12 za Ligi Kuu ya Vodacom zimepokea sh. milioni 6.6 kila moja kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Fedha hizo zinatokana na haki ya televisheni iliyopata Kampuni ya Sahara Media Group kuonesha ligi hiyo. Kampuni hiyo inayoonesha mechi hizo kupitia kituo chake cha televisheni cha Star ndiyo iliyoshinda tenda kwa sh. milioni 140.
Mkataba kati ya TFF na Sahara Media Group ni kuwa fedha hizo zitalipwa kwa awamu ambapo mpaka sasa zimelipwa sh. milioni 100. Klabu ambazo zinapata asilimia 80 ya malipo hayo ya haki za kuonesha mechi za Ligi Kuu zitalipwa tena mara malipo ya awamu ya mwisho ya sh. milioni 40 yatakapofanywa na Sahara Media Group.
Pia Sahara Media Group wataonesha mechi mbili kwa kushirikiana na Super Sport ya Afrika Kusini kwa lengo la kujiongezea uzoefu kwenye eneo hilo la kuonesha mechi moja kwa moja (live). Mechi hizo ni kati ya Azam na Majimaji itakayochezwa kesho (Machi 2) Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na ile kati ya Yanga na Simba itakayochezwa Jumamosi (Machi 5) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vilevile klabu za Ligi Kuu zimelipwa sh. milioni 5.2 kila moja kwa ajili ya nauli. Klabu hizo bado zinadai malipo ya nauli kwa ajili ya mwezi Machi. Klabu zitalipwa fedha hizo mara baada ya malipo kufanywa na mdhamini wa ligi hiyo. Fedha hizo hulipwa kwa awamu.
KOCHA RODRIGO STOCKLER
Kocha wa timu za Taifa za vijana, Rodrigo Stockler kutoka Brazil ameamua kuvunja mkataba kati yake na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na sababu za kifamilia.
Stockler amefikia uamuzi huo kwa vile baba yake amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na anahitaji uangalizi wake wa karibu. TFF imekubali ombi la Stockler kutokana na sababu alizotoa na vilevile kwa kuzingatia kuwa mkataba wake ulikuwa umebakiza miezi miwili kumalizika.
TFF inamshukuru kwa kazi aliyofanya kwa kipindi chote cha mkataba wake alipokuwa hapa nchini kuanzia Mei 2008 akifundisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na ile ya umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes).

KUINGIZA SILAHA UWANJANI
TFF inalaani kitendo cha kiongozi wa Simba, Swedi Nkwabi kuingia na silaha (bastola) Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Nkwabi ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba aliingia na bastola hiyo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Mtibwa Sugar ambapo aliwatishia wasimamizi wa mlangoni baada ya kumzuia kuingia uwanjani kwa kutokuwa na tiketi.
Hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia uwanjani na silaha ya aina yoyote isipokuwa askari polisi ambao huingia viwanjani kwa kazi ya kuhakikisha usalama unakuwepo kwa watu wote.
Tunapenda kuwakumbusha viongozi na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia uwanjani bila tiketi. Ndiyo maana TFF kama zilivyo klabu husika hulazimika kuwanunulia tiketi watu wao ambao wanaamini wanastahili kuingia bure uwanjani. Hayo ni makubaliano kati ya klabu na TFF.
MAPATO SIMBA v MTIBWA SUGAR
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya wenyeji Simba na Mtibwa Sugar limeingiza sh. 39,954,000. Watazamaji 8,609 walishuhudia pambano hilo lililochezwa juzi (Februari 27) Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kiingilio kwa VIP kilikuwa sh. 15,000 ambapo waliingia watazamaji 151, Jukwaa Kuu sh. 8,000 (watazamaji 1,465), Jukwaa la Kijani sh. 5,000 (watazamaji 2,495) na Mzunguko sh. 3,000 (watazamaji 4,498).
MAPATO RUVU SHOOTING v YANGA
Mechi namba 102 kati ya wenyeji Ruvu Shooting na Yanga iliyochezwa jana (Februari 28) kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro imeingiza sh. 11,280,000. Watazamaji 3,760 ndiyo walionunua tiketi kwa ajili ya kushuhudia pambano hilo. Mechi hiyo ilikuwa na kiingilio kimoja cha sh. 3,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari

Post a Comment

Previous Post Next Post