JUMLA ya warembo sita, wamechujwa katika kinyang’anyiro cha kumtafuta Kisura wa Tanzania 2010/11 ambacho fainali yake itafanyika Machi 18, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Mradi wa Kisura Tanzania, Juliana Urio, alisema kuwa warembo hao wamechujwa baada ya kura zilizopigwa na watazamaji wa mchakato wa shindano hilo kupitia kituo cha televisheni ya taifa (TBC 1).
“Kama ulivyo utaratibu wetu kwa miaka yote, watazamaji walipata fursa ya kuwapigia kura warembo wa kutoka na kufanya hivyo ambapo hao sita ndio waliotoka hadi sasa,” alisema.
Aliwataja waliochujwa wiki ya kwanza kuwa ni Angel Mombeki na Monica Fikiri wa Tabora, wiki ya pili ni Asha Hamis na Diana Moshi kutoka Dodoma, wakati waliochujwa wiki ya tatu ni Winfrida Sabega kutoka Dar es Salaam na Dotinata Soro wa Arusha.
Urio alisema kuwa mchujo huo utaendelea wikiendi hii kabla ya fainali ya shindano hilo linalotarajiwa kuwa na mvuto wa hali ya juu kutokana na ubora wa warembo walionao.
“Hadi sasa maandalizi yanakwenda vizuri, kinachosubiriwa ni kumpata mshindi tu hiyo Machi 18. Warembo wapo kambini katika Hoteli ya Kiromo, Bagamoyo wakifundishwa mambo mbalimbali, zaidi ikiwa ni jinsi ya kujitambua wakiwa kama wasichana wadogo wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali katika jamii,” alisema Urio.
Alisema kuwa Jumapili wanatarajia kutangaza zawadi kwa mshindi na wengineo, ukumbi pamoja na mambo mengineyo yanayohusiana na shindano hilo linalofanyika kwa mwaka wa tatu sasa.
Mdhamini mkuu wa shindano hilo ni Family Health International (FHI), TBC1, Kiromo View Resort Hotel, TanFoam (Arusha), SBC Limited, TBL kupitia kinywaji chake cha Redd’s, Flare Magazine, Hugo Domingo, BASATA, GRM Production, Clouds FM, ATCL na MJ Records.