TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kinatangaza kuwa kampuni ya utalii iitwayo Zara Tours Limited ya mkoani Arusha imejitosa kudhamini tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania Mwaka 2010.
Zara Tours itadhamini tuzo hizo kwa kumpa ziara ya siku tano atakayeibuka Mwanamichezo Bora wa Tanzania Mwaka 2010 kutembelea mbuga za wanyama za Ngorongoro na Serengeti kwa nia ya kutangaza utalii hapa nchini.
TASWA inamshukuru Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Zainab Ansell kwa udhamini huo, ambapo mshindi huyo akiwa huko yeye pamoja na mtu mwingine atakayeamua kuambatana naye watapata huduma zote za watu mashuhuri.Pia mshindi ataambatana na mwandishi wa habari mmoja.
Udhamini huo sasa umeongeza zawadi atakazopata mshindi, ambaye pia atapewa gari aina ya Toyota Cresta GX 100 kutoka kwa wadhamini Kampuni ya Bia ya Serengeti na Dekoda kutoka MultiChoice Tanzania. Pia atalala kwa siku moja hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam.
Pia naomba kutoa ufafanuzi kuwa TASWA inatafuta wanamichezo bora wa mwaka 2010 na si wa mwaka 2011 kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
Tayari orodha ya vyama ambavyo wanamichezo wake watapewa tuzo tumeshaitangaza na wengi wa wanamichezo hao wanatokana na mapendekezo ya vyama vyao ukiacha michezo michache ikiwemo soka.
Soka kama tulivyotangaza juzi kwenye mkutano na waandishi wa habari, kwamba kulikuwa na Kamati Maalum iliyoteuliwa ikiongozwa na baadhi ya wahariri wa habari za michezo na baadhi ya wajumbe wa TASWA kulingana na vigezo ambavyo vipo kwa tuzo hiyo.
Pia ieleweke mshindi upande wa soka si kwamba ndiye moja kwa moja atazawadiwa gari, maana tuzo yetu si ya Mwanasoka Bora wa Mwaka, ila kinachofanyika mshindi wa kila mchezo atashindanishwa na wenzake wa michezo mingine ili kumpata Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2010, ambaye atapewa hilo gari.
Lakini kwa vile kila mchezo una majina matatu, washindi wa kila mchezo nao watapewa zawadi ya fedha taslimu, ambayo tayari imeshatangazwa na watahesabika ni washindi wa mchezo husika mwaka 2010.
Ahsanteni.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
29/04/2011