Kama mnavyofahamu TASWA kwa kushirikiana na Shule Kuu ya
Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) inaandaa mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari za michezo
nchini.
Mchakato wa mafunzo hayo bado unaendelea kwa uratibu wa
karibu kati ya vyombo hivyo viwili, ambapo bado tunaendelea na mazungumzo na
wadhamini mbalimbali ili kuyafanya mafunzo hayo yawe bora zaidi na mazungumzo
yatakapokamilika tutawajulisha.
Kwa kuwa mafunzo hayo yatakuwa ya mara kwa mara ndiyo sababu
mchakato wake unachukua muda mrefu ili pindi yatakapoanza zile ndoto zetu za
kusaidia wanahabari wa michezo ziweze kutimia. UCHAGUZI
MKUU
Kamati ya Katiba ya TASWA inatarajiwa kukutana wiki
inayoanza kesho kwa ajili ya masuala ya katiba ya chama chetu.
Kama mnavyofahamu chama kimekuwa na utaratibu wa kufanya
uchaguzi kila baada ya miaka mitatu na tayari muda umewadia.
Hivyo tunaamini mchakato wa katiba utaenda vizuri na baada
ya kamati ya katiba kumaliza vikao vyake, Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana
kwa masuala mbalimbali ikiwemo kupanga tarehe ya mkutano wa katiba na pia
mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama mwaka huu.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
01/09/2013