FEDHA ZA EPA ZAWAPA KIFUNGO CHA MIAKA MITANO MARANDA NA FARIJALA

                                 RAJABU MARANDA MBELE NA FARIJALA HUSEIN WAKIWA KIZIMBANI






Na Happiness Katabazi


VILIO,simanzi, majonzi na huzuni kwa zaidi ya saa sita leo vilitawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, baada ya mahakama hiyo kuwa hukumu kifungo cha miaka mitano jela Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda na binamu yake Farijala Hussein kwa makosa ya kugushi nyaraka na kisha kujipatia ingizo la Sh.bilioni 1.8 isivyo halali kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.
Jopo la Mahakimu Wakazi lilokuwa likiongozwa Saul Kinemela ,Phocus Bambikya ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani na Elvin Mugeta ambaye pia ni Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ndiyo jana kuaniza saa 4;18 hadi saa 5;20 asubuhi ndiyo waliketi katika viti vitatu vya enzi katika ukumbi namba mbili wa Mahahakama hiyo na kusoma hukumu hiyo ya kwanza kati ya kesi 14 za EPA zilizofunguliwa mahakamani hapo, ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa na wananchi huku umati mkubwa wa ndugu,jamaa,marafiki na wananchi mbalimbali walifurika kusikiliza hukumu hiyo.
Hakimu Mkazi Mugeta ndiye aliyesoma hukumu ya kesi hiyo kwaniaba ya wanajopo wenzake huku akionyesha kujiamini hakimu huyo alisema kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Novemba 4 mwaka 2008 na jopo hilo lilipata fursa ya kusikiliza jumla ya mashahidi tisa wa upande wa Jamhuri ambao walifika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao na kwamba jopo hilo pia lilisikiliza utetezi uliotolewa na washtakiwa hao na jopo hilo likauchambua kwa makini.
Hakimu Mugeta aliikumbusha mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na jumla ya makosa nane.Makosa hayo ni kula njama kutenda kosa la wizi wa kiasi,kughushi hati ya kuamisha deni(deed of asssigment)inayoonyesha kampuni hewa ya washtakiwa ya Kiloloma&Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai India,kughushi hati la jina la biashara la kampuni hiyo ambayo inaonyesha imetolewa na Msajili wa Makampuni nchini (BRELA),kumbe si kweli, kuwasilisha nyaraka hizo zilizoghushiwa BoT,kuwasilisha nyaraka hizo kwenye Benki ya Afrika(BoT) na kufungua ,kujipatia ingizo la kiasi hicho cha fedha isivyo halali na wizi sh 1,864,949,294.45 .
“Baada ya kupitia hati makosa hayo yote katika hati ya mashtaka na kupitia ushahidi na utetezi uliotolewa na pande zote mbili, jopo hili limefikia uamuzi wa kutia hatiani washtakiwa hao kwa shtaka la pili,tatu,nne,tano,sita na saba.Na kwamba mahakama hii imeshinedwa kuwatia hatiani kwa kosa la kwanza ambalo ni kula njama na kosa la nane ambalo ni la wizi kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kwamba washtakiwa hao walikula njama na kuiba katika BoT”alisema Hakimu Mugeta huku ndugu na jamaa wakijifuta machozi ndani ya chumba cha mahakama.
Mugeta ambaye alikuwa akisoma hukumu hiyo huku akinywa maji ya kunywa maji alisema jopo hilo linakubalina na ushahidi wa upande wa Jamhuri kuwa washtakiwa hao walighushi nyaraka hizo kwasababu mashahidi watatu wa Jamhuri ambao ni Ofisa wa Polisi-Salum Kisai,Ofisa Mkurugenzi Mtendaji wa BRELA, Esteriano Mahingira katika ushahidi wao waliweza kuithibitishia mahakama kuwa nyaraka hizo zilikuwa zimeghushiwa.Mahingira katika ushahidi wake aliidhibitishia mahakama kuwa saini iliyokuwa kwenye hati ya jina la biashara ya Kampuni ya Kiloloma&Brothers ambayo washtakiwa wanadai ni yake,siyo yake.Na Kisai kwa upande wake ndiyo alichukua maelezo ya onyo kwa washtakiwa ambao walikiri kutenda makosa hayo na maelezo hayo yalipokelewa na mahakama na vielelelezo.
“Na kwa mujibu wa utetezi wa Maranda na Farijala wao walijitetea kuwa siyo wao walioandaa nyaraka hizo ambazo Jamhuri inadai ziliandaliwa na na kwamba Charles Issack Kissa maarufu kwa jina la Chares ni jina la kufikirika…na na Farijala akadai kuwa nyaraka zote hizo ziliandaliwa Chares siyo yeye; Sasa mahakama hii imejiuliza kwamba kesi inayowakabili washtakiwa ni nzito na kwamba kama mkubwa na ni kwanini washtakiwa hao wasingemleta huyo Chares kama shahidi wao ili awatete? Na kwakuwa hilo la kumleta Chares halikufanywa na washtakiwa, mahakama hii inakubaliana na upande wa Jamhuri kuwa Chares ni mtu wa kufikirika na kwamba Chares ni Farijala ambaye ndiye aliyeandaa na nyaraka zote hizo ambazo zimegushiwa ambazo zilitumiwa na washtakiwa wote kujipatia ingizo hilo la fedha”alisema Hakimu Mugeta hukumu ndugu na jamaa waliokuwa wakifuatilia hukumu hiyo wakijifuta machozi na wengine kutoka nje na kurudi ndani ya chumba cha mahakama kuendelea kusikiliza hukumu hiyo.
Aidha Hakimu huyo akiendelea kuchambua hukumu hiyo alisema katika utetezi wa washtakiwa wenyewe kwa hiari yao walikiri kuwa wao ni wamiliki wa kampuni ya Kiloloma&Brothers na kwamba ni kweli ndiyo waliofungua akaunti ya pamoja katika Benki ya Afrika na kuwa walikiri kuwa walijipatia ingizo la kiasi hicho cha fedha toka BoT na kwamba katika utetezi wake Maranda alidai mahakamani hapo kuwa alihusika na mchakato wa kudai deni hiyo na kwamba ni kweli alipewa idhini ya kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai India kudai deni lake na kwamba alichokizingatia yeye ni kupata kiasi hicho cha fedha na siyo kutazama uhalali wa hizo nyaraka alizotumia kupata fedha hizo toka BoT.
Hakimu Mugeta alisema utetezi huo wa washtakiwa jopo hilo umeukataa kwasababu hauna msingi kwasababu ushahidi wa Maranda na Farijala unakinzana hivyo mahakama hiyo inakubalina na upande wa jamhuri kwamba ni kweli washtakiwa hao na watu wengine wasiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam mwaka 2005 walighushi nyaraka hizo ambazo zilisababisha wajipatie ingizo hilo la fedha.
Baada ya kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa makosa hayo jopo hilo lilitoa fursa kwa upande wa Jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Stanslaus Boniface na Shadrack Kimaro na Upande wa Utetezi uliokuwa ukiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu kusema lolote kama wanalo kabla ya mahakama hiyo haijatoa adhabu kwa washtakiwa.
Wakili Mkuu wa Serikali Boniface alieleza mahakama kuwa kwa kumbukumbu zilizopo zinaonyesha hii ni mara ya kwanza washtakiwa hao kutiwa hatiani na mahakama na kwamba mahakama hiyo sasa ione haja ya kutoa adhabu kali kwasababu kiasi cha fedha kilichopotea ni kikubwa na kimeleta madhara kwa wananchi na akaiomba mahakama itumie kifungu cha 358(1)cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002; itoe amri kwa washtakiwa warejeshe kiasi hicho cha fedha kwa mwenye fedha hizo ambae ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake wakili Magafu aliomba mahakama iwaonee huru washtakiwa kwani hii ni mara ya kwanza wanatiwa hatiani ,ni wagonjwa wa figo, wanategemewa na familia na makosa mengine waliyotiwa nayo hatiani waliyatenda bila kujua au kutoelekezwa vyema na taasisi husika na kuongeza kwa kuiomba mahakama hiyo itumie kifungu cha 38 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 ambacho kinasema kuwa pamoja na mahakama kumtia mshtakiwa hatiani ,basi mahakama inaweza inaweza kumwachiria huru kwa masharti hivyo wanaomba jopo hilo likiwa linatoa hukumu hiyo ikiangalia kifungu hicho.
Akisoma adhabu baada ya kusikiliza maombi hayo mawakili wa pande mbili, Hakimu Mkazi Mugeta alisema jopo hilo limesikiliza maombi washtakiwa kupitia kwa wakili wao Magafu na kwamba jopo hilo limezingatia katika adhabu wanayotaka kuitoa pia wamezingatia uzito wa makosa yaliyofanywa na washtakiwa ambayo jopo hilo limewakuta na hatia na kwamba kosa la pili ambalo washtakiwa wote wamepatikana na hatia ambapo kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Mugeta alisema kosa la tatu ambalo washtakiwa wote wawili wametiwa nalo hatiani kila mmoja wao atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.Kosa nne ambalo washtakiwa wote wametiwa hatiani pia kila mshtakiwa atatumika miaka mitano jela.Kosa la tano ambalo ni mshtakiwa wa pili peke yake(Maranda) ndiyo amepatikana na hatia na atatumikia miaka miwili jela.Kosa la sita ambalo washtakiwa wote wametiwa hatiani ambapo kila mmoja wao atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela na shtaka la saba ambalo pia washtakiwa wote wawili wamepatikana na hatia wanatatumika miaka miatatu jela.Hivyo jumla ni miaka 21 na adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja ambapo washtakiwa hao watatumikia miaka mitano jela.
Baada ya hakimu huyo kumaliza kusoma hukumu hiyo, yeye na mahakimu wenzake waliondoka ndani ya ukumbi wa mahakama na kufanya ndugu,jamaa na familia za washtakiwa wakiangua vilio kwa sauti ya juu na askari polisi na waliwatoa kizimbani washtakiwa hao na kuwapeleka kwenye mahabusu ya mahakama hiyo kwaajili ya kusubiri taratibu nyingine za kiutawala zifanyike ili washtakiwa waweze kupelekwa gerezani.
Washtakiwa hao tangu saa 5:22 asubuhi waliifadhiwa kwenye mahabusu ya mahakama hiyo huku Tanzania Daima ikishuhudia ndugu wa washtakiwa hao wakihaha huku na kule na wengine kwenda kwenye maduka ya jirani kununua maji, dawa za miswaki,sabuni na maziwa kwaajili ya kuweza kuwapatia ndugu zao ambao ilipofika saa 9:30 alasiri gari aina ya Toyota Land Cruser lenye Namba za usajili SCN 9008K, mali ya Jeshi la Polisi, huku askari kanzu na wale waliokuwa wamevalia sare wakiwa wamebeba silaha nzito mabegani na wengine kuvalia viuno kwaajili ya kuimarisha ulinzi, waliwapakisha wafungwa hao kwenye gari hilo la wazi ambao waliketi nyuma mithili ya ‘maharusi’ ambapo wakati gari hilo lilivyokuwa likitoka ndani ya viwanja vya mahakama hiyo wafungwa hao walikuwa wakipunga mikono kwa umati uliokuwa umefurika kwenye viwanja vya mahakama hiyo huku ndugu na jamaa na wake zao wakiangua vilio na kulisindikiza gari hilo hadi nje ya lango la mahakama hiyo.
Baadhi ya wananchi na mawakili waliofika mahakamani hapo walitoa maoni hayo wakisema hukumu hiyo ni ndogo ukilinganisha na kiasi cha fedha kilichochukuliwa na wafungwa hao,waliipongeza ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP),Eliezer Feleshi na timu yake kwa kazi nzuri iliyosababisha wafungwa hao kutiwa hatiani huku baadhi ya mawakili wanaotetea washtakiwa wengine wa kesi za wizi wa EPA, wakisema hukumu hiyo ni ishara mbaya kwa wateja wao na kwamba hukumu hiyo hivi sasa imethibitisha kesi za EPA siyo usanii ni ukweli.
Jumla ya kesi 14 za EPA zilifunguliwa na DDP- Feleshi kwa kishindo kwa mara ya kwanza Novemba 4 mwaka 2008 dhidi ya washtakiwa mbalimbali wakiwemo mfanyabiashara maarufu nchini Jayantkumar Chandubhai Patel ‘Jeetu Patel na wenzake na baadhi ya maofisa wa BoT ambao bado kesi zao zinaendelea kusikilizwa mahakamani hapo.
Mbali na kesi hiyo Na.1161/2008 ambayo jana ilitolewa hukumu, Maranda na Farijala pia wanakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa Sh milioni 207 ambapo anashtakiwa yeye na maofisa wa BoT, Mkuu wa Idara ya EPA, Iman Mwakosya na Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo Ester Komu, na Katibu wa Benki Bosco Kimela.
Katika kesi hiyo ya wizi Maranda anadaiwa kutumia nyaraka za kughushi kuonyesha kampuni yake ya Rashaz Tanzania kuwa imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Rashaz T Ltd na kisha kujipatia ingizo hilo la Sh milioni 207 huku akijua si kweli.
Kesi ya tatu ya jinai ni kesi Na. 1164/2008 ya wizi wa shilingi bilioni 3.8 katika akaunti hiyo ambayo inasikilizwa mbele ya jaji Beatrice Mutungi, Hakimu Mkazi Samwel Karua na Elvin Mugeta. Katika kesi hiyo, washitakiwa Farijala, Maranda, Iman Mwakosya, Ester Komu, Ajay Somani na Sophia Lalika walitumia kampuni ya Mibale Farm kuonyesha imepewa idhini ya kudai deni la kampuni ya Lakshmi Textile Mills co. Limited ya India huku wakijua si kweli.
Juni 11 mwaka 2009, mahakama hiyo ilimuona Maranda na Farijala ambao wanakabiliwa na jumla ya kesi nne za wizi katika EPA, kuwa wana kesi ya kujibu katika kesi Na.1161/2008 ambayo ilitolewa hukumu jana na kwamba upande wa Jamhuri unaowakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface aliyekuwa anasaidiwa na Timon Vitalis, Frederick Manyanda na Shadrack Kimaro umeweza kuthibitisha kesi yao.
Juni 6 mwaka 2009, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Boniface aliwasilisha majumuisho ya kesi hiyo akiiomba mahakama hiyo iwaone washtakiwa wote hao wana kesi ya kujibu, kwani Jamhuri imeweza kuthibitisha kesi hiyo na kwa hiyo washtakiwa hao wana kila sababu ya kujibu kesi inayowakabili.
Aidha, Aprili 29 mwaka 2010, Rajabu Maranda alipanda kizimbani kutoa utetezi wake katika kesi hiyo ambayo leo inatolewa hukumu ambapo aliieleza mahakama hiyo kuwa alichokuwa akikizingatia katika mchakato wa kudai deni katika (EPA) ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.

Post a Comment

Previous Post Next Post