Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kufungua msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom
2011/2012 kati ya Yanga na Simba iliyokuwa ichezwe Agosti 13 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, sasa itafanyika Agosti 17 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Uamuzi huo umetokana na timu ya Taifa (Taifa Stars) kuwa na mechi ya kirafiki
katika kalenda ya FIFA (FIFA dates) ugenini itakayochezwa Agosti 10 mwaka huu
dhidi ya Palestina. Stars itarejea nchini Agosti 11 mwaka huu baada ya mechi
hiyo.
Wachezaji wengi wanaounda kikosi cha Taifa Stars kwa sasa wanatoka katika klabu
hizo mbili. Awali Stars ilikuwa icheze mechi nyingine Agosti 13 mwaka huu jijini
Amaan wakati aikitokea Palestina. Kocha Mkuu wa Stars, Jan Poulsen ameifuta
mechi hiyo kwa vile Jordan haitakuwa na wachezaji wake wa kulipwa kutokana na
kuwa nje ya kalenda ya FIFA.
FAINALI LIGI YA TAIFA
Fainali ya Ligi ya Taifa itakayoshirikisha timu 12 zitakazogawanywa katika
makundi matatu ya timu nne nne itafanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga
kuanzia Agosti 6 mwaka huu.
Awali ligi hiyo ilianza katika vituo vinne ambapo timu tatu za juu ndizo
zilizopata tiketi ya kucheza fainali. Kituo cha Pwani kimetoa timu za
Cosmopolitan (Ilala), Sifapolitan (Temeke) na Mgambo Shooting (Tanga) wakati
Samaria (Singida), Majengo SC (Dodoma) na Morani (Arusha) zimefuzu kutoka kituo
cha Singida.
Police Central (Ilala), Small Kids (Rukwa) na JKT Mlale (Ruvuma) zimefuzu kutoka
kituo cha Rukwa wakati kituo cha Kigoma kimetoa timu za Kasulu United (Kigoma),
Geita Veterans (Mwanza) na Rumanyika SC (Kagera).
Timu zinatakiwa kuwasili Tanga siku mbili kabla ya fainali kuanza ambapo mshindi
wa kwanza katika kila kundi pamoja na washindwa bora (best losers) wawili
watapanda hadi daraja la kwanza.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF