Kamati ya Rufani ya TFF iliyokaa Julai 23 mwaka huu imesikiliza rufani
iliyokatwa na Mwamuzi wa Daraja la Kwanza, Kamwanga Tambwe. Baada ya kuangalia
nyaraka zilizotolewa kwenye kamati, kumsikiliza na kumhoji, kamati imefikia
uamuzi ufuatao;
Kamati ya Rufani imeona rufani hii haina msingi, na hivyo kutoa adhabu
zifuatazo;
1. Kumfungia Mwamuzi Kamwanga Tambwe kutojihusisha na masuala ya mpira wa
miguu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Oktoba 20, 2009 kulingana na Ibara ya
45 (ii) ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikisomwa pamoja
na Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Ibara
ya 62(ii).
2. Fedha shilingi laki mbili (200,000/-) zilizohusishwa na rushwa katika
shauri hili, kufuatana na kifungu 62(iv) cha Kanuni za Nidhamu za FIFA zibaki
TFF kwa shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu.
Imesainiwa na Wajumbe wa Kamati ya Rufani;
Prof. G. Mgongo Fimbo - Mwenyekiti
Dk. Ong’wanuhama Kibuta - Makamu Mwenyekiti
Lt. Kanali mstaafu Idd Kipingu - Mjumbe
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jamal Rwambow - Mjumbe
Henry Tandau - Mjumbe
Taarifa za nyongeza (background information);
Tambwe na wenzake walifungiwa maisha na Kamati ya Mashindano ya TFF kwa tuhuma
za kupokea rushwa kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Majimaji ya Songea
na Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyochezwa mwaka 2009. Awali walikata rufani Kamati
ya Nidhamu ya TFF ambayo iliwapunguzia adhabu hiyo hadi miaka mitatu. Tambwe kwa
upande wake hakuridhika na uamuzi huo, hivyo kukata rufani Kamati ya Rufani ya
TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)