TFF YAZIKAANGA SIMBA NA YANGA


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limezinyooshea kidole timu zote zilizowatoa wachezaji wake kwa mkopo, likisema kama hakukuwa na makubaliano baina yao na klabu waendazo halitabariki uhamisho huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura (pichani), alisema kuwa, suala la kumpeleka mchezaji kwa mkopo kwenye timu nyingine, ni lazima kuwe na makubaliano ya maandishi na mchezaji husika aridhie.
Alisema, kwa hili linalosemwa kwa Simba na Yanga kwamba, zimewapeleka wachezaji kwa mkopo katika timu nyingine bila ridhaa, hadi baadhi yao kutishia kutocheza tena soka msimu huu, halikubaliki.
Wambura alisema, iwapo timu hizo zitakuwa zimekiuka utaratibu huo na kutoa uamuzi bila kuwashirikisha wachezaji hao na wakakataa kwenda, TFF itawahesabu kuwa ni wachezaji wa timu yenye mkataba nao, hivyo itawaidhinisha kuzichezea katika msimu ujao wa Ligi.
“Kesho (leo), ndio siku ya mwisho wa usajili kama timu hizi zitakuwa hazijaafikiana na wachezaji zinazotaka kuwatoa kwa mkopo, sisi tutawaidhinisha kuzichezea timu hizo ambazo wana mkataba nazo, kwa sababu kiutaratibu klabu zinapaswa kuwashirikisha, katika hatua zote na wakubaliane kwa maandishi,” alisema.
Alisema iwapo hakutakuwa na makubaliano ya pande zote tatu kwa maandishi, kuna urahisi wa mkataba kukiukwa kitu ambacho TFF haitakubali kitokee.

Post a Comment

Previous Post Next Post